[Mabadiliko] Uchambuzi; Spika Sitta Anakwenda Kufanya Kosa Kubwa..

Wednesday, March 26, 2014
Na Maggid Mjengwa,

IMETOLEWA hoja bungeni. Mtoa hoja ni Julius Mtatiro, anasema; "Kwa sababu Rais alikaribishwa tu kwa heshima kwenye bunge hili kuja kufungua na sasa akaanza kujibu ile hotuba, hatuoni kama kuna haja ya kujenga utaratibu wa kumleta tena mtoa hoja ili na yeye aje kujenga hoja juu ya maswali aliyoeleza Rais?"- Julius Mtatiro.

Spika Samwel Sitta naye akasimama kusema kuwa kuna wajumbe waliotaka hotuba ya Rais bungeni na uwasilishaji wa ripoti ya Tume uliofanywa na Jaji Warioba ujadiliwe bungeni. Hivyo, kwa busara na hekima yake Spika Sitta akatamka kuwa ataandaa siku ya wajumbe kujadili hotuba ya Rais na kilichowasilishwa na Jaji Warioba.

Kwa mtazamo wangu, haya ni makosa makubwa yatakwenda kufanyika bungeni . Na Spika Sitta , kwa kutanguliza busara na hekima zake, bado ana nafasi ya kuyaepuka makosa haya. Maana, nitakuwa mtu wa mwisho kushangaa, kama kitachotokea Bungeni kitasababisha mtafaruku mkubwa kuliko hayo maridhiano anayodhani Spika kuwa yatapatikana. Kwamba yatakayotokea yanaweza yasiliache Bunge salama. Yatazidisha mgawanyiko zaidi hata nje ya Bunge. Yaweza kuwa mwanzo wa kujenga misingi ya kuvunjika kwa Bunge lenyewe. Yangu ni tahadhari tu.

Maana, kwa kuruhusu wajumbe kuwajadili Rais na Warioba tutarajie malumbano ya kishabiki yaliyochanganyika na nderemo, mipasho na hali ya kugonga meza bila utaratibu. Kama aibu hiyo ya taifa ndiyo Spika Sitta anataka Watanzania waishuhudie , basi, hakuna shaka itakuwa ni zaidi ya aibu. Ni vituko tulivyokwisha ziona ishara zake hata kabla bunge hili kuanza.

Kwanini nasema hivi? Nionavyo hakukuwa na sababu ya msingi ya kuyarudisha bungeni malumbano ambayo tayari yameshatokea na hata kuwagawa wajumbe na Watanzania. Tayari mtazamo uliopo ni kuwa wabunge wanakwenda kuwajadili Rais Kikwete na Jaji Warioba. Hakutakuwa na kujadili hoja bali kuleta vioja. Alichosema Mheshimiwa Rais kimsingi ni maoni yake. Ana haki pia ya kutamka hisia zake. Na Rais aliweka wazi kuwa maamuzi ya mwisho ni ya wajumbe wenyewe. Kwanini sasa wajumbe wajadili maoni ya Rais? Huko kunaweza pia kutafsiriwa kuingilia kazi ya Tume ya Katiba. Na hakuna mantiki ya kumjadili Warioba kwa vile alichowakilisha si mawazo yake bali ni ripoti ya Tume iliyotokana na maoni ya wananchi. Ufafanuzi wa alichowasilisha Warioba unaweza kufanywa hata na wajumbe wengine wa Tume, si lazima Jaji Warioba.

Hofu yangu nyingine ni kuwa mjadala kama huu utakaoishia kuwajadili watoa hoja badala ya hoja walizowasilisha utapelekea kuanza hata kumwita majina Rais wa nchi. Tukubaliane, kuwa Rais wa nchi, awe ametoka chama chochote kile, anabaki kuwa ni Rais wa nchi na anastahili kuheshimiwa hata kama si wote wenye kukubaliana na maoni yake.

Msingi hapa ni kutambua na kuheshimu mambo makubwa mawili katika demokrasia. Kuwa kwenye jamii yeyote ile, pasipo na uhuru wa kujieleza na pasipo na utii wa sheria, basi, hakuna demokrasia.

Kila mtu aweze kusema kwa uhuru kabisa. Na si kusema tu, asikilizwe anachosema. Hata kama mawazo yake hayapendwi kiasi gani.

Wenye fikra tofauti, hata wakiwa wachache ni vema wakasikilizwa. Ni haki yao. Fikra zao ziruhusiwe na zishindwe tu kwenye majadiliano ya hoja. Na hata wakishindwa kwa hoja, uhuru wao wa kuendelea kujadili jambo waliloshindwa lazima uheshimiwe na ulindwe. Maana, wachache hao wanaweza kuyapanga upya mawazo yao na hata kufanikiwa kuwashawishi walio wengi kukubaliana nao.

Na walio wengi nao wana haki ya msingi ya kuyasimamia mawazo yao hata pengine kuwaridhisha wachache kuwa kilichoamuliwa kwa mawazo ya wengi ni sahihi. Maana, siasa ni majadiliano endelevu ya hoja na si kugombana kwa kutiana kabali au kutishana.

Na katika kulumbana huko kwa hoja kuna wakati lazima kulumbana huko kukatishwe na maamuzi yafanyike. Bila hivyo hakutakuwa na kazi yoyote inayofanyika isipokuwa kulumbana tu.

Kama ilivyo, kuwa walio wachache ni vema wakasikilizwa, mawazo ya walio wengi hayana budi pia kuheshimiwa. Maana, uamuzi utakaotolewa utakuwa umetokana na mawazo ya walio wengi. Utakuwa ni uamuzi wa watu na si kikundi kidogo cha watu.

Na kwa vile maamuzi yenye kutokana na matakwa ya wengi ndio yenye kufanya sheria, basi, la pili la muhimu katika demokrasia ni utii wa sheria. Ni lazima kila mmoja atii sheria, ni pamoja na wale walioipinga kabla ya kupitishwa na wengi kwa kufuata misingi ya kidemokrasia.

Maggid Mjengwa,
Iringa
0754 678 252
http://mjengwablog.com

--
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la ‘Mabadiliko’.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
 
 
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/CAMD-ye7g1t33E%2BwsE6o3i%3DWV%3DmsmMdr9ewuf6J3PMd0%3DLExDFQ%40mail.gmail.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments