[Mabadiliko] Neno La Leo: Bunge La Katiba Na ' Vifungu Vya Kifo!'

Thursday, March 06, 2014
Ndugu zangu,

Watanzania leo tunavuta pumzi huku tukielekeza macho na masikio yetu katikati kabisa ya nchi yetu tuliyozaliwa na tunayoipenda. Ni Dodoma.

Huko itapatikana leo hatma ya mwelekeo wa mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya ya Nchi Yetu.

Hata hivyo, kuna ishara mbaya kuwa tuliowatuma Dodoma wako katika hatari ya kukwamisha mchakato mzima kwa kujikita kwenye kupigania kisicho na maslahi ya nchi hii kwa miaka 50 au 100 ijayo.

Watapigania yaliyomo kwenye vifungu vya 36 mpaka 37 za Kanuni za kuendesha Bunge hilo Maalum. Inahusu namna watakavyofikia maamuzi, kuwa iwe ni kwa kura za faragha au dhahiri. Ndio, inahusu kura za siri au kura za wazi. Ni' vifungu vya kifo' maana ndivyo vitakavyoamua, kwa namna moja au nyingine, uhai wa mchakato mzima wa kuitafuta Katiba.

Tuliowatuma Dodoma wamejigawa katika makundi ya ' Sisi' na ' Wao'. Wanatafuta kushindana na kupata mshindi badala ya kutafuta muafaka wa Kitaifa. Na hakika, kama alivyopata kusema Rais wa Nchi, Jakaya Kikwete, kuwa kwenye kushindana huko hakuna atakayeshinda. Tutashindwa Sote. Na huo ndio UKWELI.

Hakika, huu ni mtihani mgumu ulio mbele yao tuliowatuma Dodoma. Wakishindwa mtihani huu, basi, ishara zinazoonekana ni za mkwamo wa jumla wa mchakato mzima. NI AIBU.

Tuliowatuma Dodoma hawajachelewa kuitafuta hekima na busara kutunusuru na aibu kubwa ya taifa iliyo mbele yetu. Tuliowatuma Dodoma wawafikirie pia watoto wa kesho na wa vizazi vijavyo katika nchi yetu tuliyozaliwa na tunayoipenda.

Na ushauri hapa ni heri kukubaliana kutokubaliana, na hivyo, kusitisha kwa muda mchakato huo, kuliko kulazimisha kwenda mbele. Ni ushauri pia, kuwa ni heri kuyatafuta maridhiano kwanza kabla ya kuingia kwenye majadiliano, kuliko kuyatafuta maridhiano baada ya kuingia kwenye mapigano na kujeruhiana. Ni busara basi, tuliowatuma Dodoma wakaunda Kamati Maalum ya kuyatafuta maridhiano wa vifungu hivyo. Na ifahamike, kuwa MARIDHIANO ndio msingi wa UHALALI wa mchakato na hata Katiba yenyewe.

Tusipotanguliza busara, hekima na maslahi ya taifa, yumkini yaweza ikawa kama yale aliyopata kuyasema miaka 60 iliyopita, mwandishi yule mahiri, Mtanzania mwenzetu Shaaban Robert, aliandika; ” Wasadikika wana desturi ya kutafuta fimbo baada ya kuumwa na nyoka. Tumekwisha umwa na nyoka wa matendo yetu mabaya ya zamani.

Nyoka mwenyewe amekwishakimbia. Hapatikani kwa kujilipiza kisasi, lakini, sumu yake imebakia katika jeraha tulilolipata. Sasa, shauri lililo jema ni kuzuia sumu hii isienee miilini mwetu ikaleta kifo.

Maovu yana hatari kubwa kukaa kati yetu. Tumedumu nayo kwa muda mrefu. Hayakutuletea faida ila hasara, huzuni na kilio siku zote.”- Shaaban Bin Robert.

Ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa,
0754 678 252
http://mjengwablog.com

--
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la ‘Mabadiliko’.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
 
 
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/CAMD-ye5n-UUyH2UC%2BmGeaYPPEXSRRxv7JbU7efrSf_kmSv7OaA%40mail.gmail.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments