[wanabidii] Taarifa ya MSD kuhusu utaratibu wa manunuzi ndani ya bohari ya dawa

Thursday, February 20, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UTARATIBU WA MANUNUZI NDANI YA BOHARI YA DAWA


Idara ya Bohari ya Dawa (MSD) iliundwa kwa sheria ya Bunge Na. 13 ya mwaka 1993. Ni Idara inayojitegemea chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo ilianzishwa ili kuunda, kudumisha na kusimamia mfumo ulio bora na wenye gharama nafuu wa ununuzi, uhifadhi na usambazaji dawa na vifaa-tiba, vitendanishi kwa ajili ya hospitali navituo vya kutolea huduma ya afya nchini

Takwimu zilizopo kwa sasa zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia Themanini (80%) ya mahitaji yote ya Dawa,Vifaa tiba, Vitendanishi nchini vinatoka nje ya nchi hivyo taratibu za manunuzi hufuata taratibu na miongozo ya ndani ya nchi na ya kimataifa.

Utaratibu wa uagizaji na uingizaji wa dawa ndani ya nchi huratibiwa na kusimamiwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), kuwa dawa yoyote kabla ya kuingizwa chini lazima iwe imesajiliwa na Mamlaka na hukaguliwa pindi inapogombolewa ili kuhakikisha ubora wake. Sambamba na ukaguzi huo pia Bohari inavyo vitengo vya Ukaguzi wa Ndani (Internal Audit) na Uthibiti Ubora (Quality Assurance) ili kujihakikishia zaidi kuwa taratibu za manunuzi zinazingatiwa pia dawa zinazonunuliwa zinakidhi viwango vilivyokwishawekwa.

Aidha taribu za manunuzi katika Bohari kama ilivyo taasisi nyingine yoyote ya Serikali husimamiwa na kuongozwa na sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 na

kanuni zake za mwaka 2013. Taratibu za manunuzi huanza pale ambapo kuna uhitaji wa dawa fulani kutoka katika vituo vya kutolea huduma ya afya nchini. Mahitaji ya dawa kutoka katika vituo vya kutolea huduma ya afya huenda sambamba na mgawo wa fedha kwa kila kituo husika. Bohari inayo Bodi 

ya Zabuni (MSD Tender Board) kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma yenye wajumbe ambao ni wafanyakazi katika Bohari wa ngazi za juu na wenye utaalamu tofauti. Bodi ya Manunuzi
ndiyo chombo cha juu chenye maamuzi ya manunuzi ndani ya Bohari hivyo manunuzi yote ndani ya Bohari husimamiwa na Bodi hii.

Njia inayotumika katika manunuzi ya bidhaa ndani ya Bohari ni kwa kupitia zabuni za kimataifa na hii ni kutokana na ukweli kwamba zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa hutoka nje ya nchi. Zabuni ya kimataifa iko wazi kwa kila mshitiri ndani na nje ya nchi bila kubagua nchi anayotoka. Kigezo cha kwanza kwa mshitiri kushiriki katika zabuni ni kuwa na bidhaa yake imesajiliwa nchini na mamlaka zinazohusika na kigezo hiki cha kusajili hakina kinga kwa mshitiri yoyote yule.

Utangazaji wa zabuni hufuata na kutumia njia na machapisho ya kitaifa na Kimataifa kupitia tovuti (webistes) za Bohari (www.msd.or.tz) na ya Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (www.ppra.go.tz). Aidha tunatumia Magazeti ya kimataifa, na ya kitaifa katika lugha za Kiingereza na Kiswahili ili kuwafikia watu wote. Zabuni hufunguliwa hadharani kwenye siku ambayo ilitamkwa kwenye gazeti na washitiri au wawakilishi wao hualikwa kwenye zoezi hilo ili kujiridhisha kuwa vigezo mbalimbali ikiwapo bei iliyotamkwa na uwepo wa nyaraka muhimu vimefuatwa.

Baada ya ufunguzi hufuata mchakato wa tathmini (evaluations) kwa kutumia wataalamu huru kulingana na zabuni husika, wakati mwingine wataalam hao hutoka nje ya Bohari kulingana na utaalam wao katika zabuni husika.

Baada ya mchakato wa tathmni hufuata zoezi la kuwapata washindi , zoezi ambalo hufanywa na Bodi ya zabuni. Washindi hupatikana kutokana na vigezo vilivyoweka na hupaswa kutimizwa. Washitiri wote hupewa mrejesho juu ya mchakato mzima jinsi ya zabuni ilivyokwenda na matokeo yake. Bohari hutumia mfumo uliowazi, haki na usawa katika manunuzi ili kuhakikisha kunakuwa na ushindani na thamani fedha kwenye mali ya umma.

Sheria ya Manunuzi ya Umma inalinda haki za mshindani yeyote yule ambaye baada ya kwisha mchakato anaweza kuwa na hisia kuwa Bohari ya Dawa haikumtendea haki kwani inamruhusu kukata rufaa kwenye Mamlaka ya ya Manunuzi ya Umma (PPRA) ambao huitisha nyaraka zote toka Bohari na kuzipitia na kisha huzitolea maamuzi.

Ili kuhakikisha uwazi na haki, Sheria ya manunuzi inatutaka tuchapishe katika vyombo vya habari matokeo ya washindi wa zabuni wote kila mwisho wa mwaka. Taarifa ya zabuni yamwaka wa fedha wa 2012/ 13 iliiyotolewa kwenye Mwananchi la tarehe 27/ 12/ 13 na la The Guardian la tarehe 31/ 12/ 13 nairudia hapa ili kuonyesha washindi wa zabuni hizo, thamani na nchi ambazo makampuni hayo yanatoka.



Kwa ufupi wafanya biashara wa Tanzania walipata mikataba 41 wakifuatiwa na India 19, Kenya 6, UAE 4, UNITED Kingdom 3, Uganda, Netherlands, Germany na China 2 kila moja, South Korea na Denmark I kila moja. Kwa hiyo wafanya biashara kutoka Tanzania walipata zaidi ya 50% ya mikataba yote.

Shughuli zote za manunuzi hukaguliwa kila mwaka na wakaguzi kutoka ofisi ya PPRA na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).

Imetolewa na

Cosmas Mwaifwani
Kaimu Mkurugenzi Mkuu

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

0 Comments