[wanabidii] Tunahitaji mbadala wa CCM na CHADEMA

Friday, January 17, 2014
Na Kitila Mkumbo

ITACHUKUA muda kuelewa nini hasa kilichokikumba Chama Kikuu cha Upinzani nchini (CHADEMA) hadi kikashindwa kutatua mgogoro wa uongozi na hatimaye kuingiza nchi katika kizungumkuti cha kisiasa tunachokishuhudia leo. Binafsi, kama mmoja ya wahusika wakubwa katika mgogoro huu nimepokea pole, lawama, na kwa kiasi fulani hongera kwa kumudu kuhimili mikikimikiki iliyonikumba. Nimepokea pole kutokana na misukosuko niliyokumbana nayo katika sakata hili hadi kufikia kufukuzwa uanachama.

Hili si jambo dogo katika maisha ya binadamu. Kufukuzwa katika ushirika wowote ni jambo linalosababisha mfadhaiko na ninazipokea pole nilizopewa kwa unyenyekevu. Ninashukuru pia kwa wale walionitia moyo kwamba hii ni ajali katika safari na nisikate tamaa katika kutoa mchango wangu katika harakati za mabadiliko ya kisiasa nchini. Nami nawaahidi kwamba bado nipo imara na nitaendelea kushiriki kikamilifu katika harakati za kuleta mabadiliko ya kisiasa hapa nchini, ndani na nje ya vyama vya siasa.

Walionipa lawama ni wale waliokubaliana mia kwa mia na viongozi wa CHADEMA waliotujengea taswira ya usaliti na uhaini kwa chama kwa uamuzi wetu wa kuandaa mkakati wa kushinda uchaguzi ndani ya CHADEMA; mkakati ambao ulikuja kutafsiriwa kama mkakati wa mapinduzi ya uongozi halali ndani ya chama. Na kwa kuwa viongozi waliongea sana na kulirudia jambo hili mara kwa mara, na kwa kuwa jamii yetu imejengwa katika kuamini uongozi zaidi kuliko mtu mwingine yeyote, wapo watu wengi ambao wameafikiana na tafsiri ya uongozi kwamba waraka ule ulikuwa ni mkakati wa mapinduzi na haukuwa na nia njema.

Wapo pia wananchi walionilaumu kama sehemu ya uongozi wa chama kwa kushindwa kuyamaliza mambo yetu ndani ya chama. Na wengine wamenilaumu kwa kutokuwa na moyo wa kubali yaishe, kwamba ningekubali kosa, hata kama siamini kwamba ni kosa, ili niombe msamaha yaishe, tusonge mbele. Natamani ingekuwa rahisi hivi na kwamba kungekuwa na nia njema kwa pande zote mbili, pengine neno samahani lingetosha kumaliza mgogoro huu.

Kwa sababu hii nazipokea lawama zote kwa unyenyekevu pia na ninakubali kwamba nimeshiriki, bila kutarajia, kusababisha usumbufu na kutatiza tamanio na tumaini la mamilioni ya Watanzania katika kuitoa CCM madarakani. Hata hivyo, taswira ya mgogoro huu ni pana kuliko inavyoonekana na pengine tutapata nafasi nzuri zaidi mbele kueleza vizuri kilichotokea katika maandishi ili watu waelewe na waielewe CHADEMA na viongozi wake vizuri, na kuweka kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

Sitarajii katika makala haya kukidhi kiu ya watu wengi wanaotamani kujua ukweli wa mgogoro ndani ya CHADEMA na pengine mimi siye mtu sahihi kueleza jambo hili kwa kuwa nina maslahi ya moja kwa moja. Ninatoa changamoto kwa watafiti wa sayansi ya siasa kulifanyia utafiti jambo hili na kuliweka bayana, ili watu wapate kujifunza na kulijua vizuri.

Nieleze tu kwamba mgogoro huu unatukumbusha kuwa, pamoja na kwamba tupo katika mfumo wa vyama vingi, bado tumeendelea kuukumbatia utamaduni wa chama kimoja. Kwa hiyo tuna vyama vingi vya siasa, lakini vyama hivi bado vinakumbatia utamaduni wa chama kimoja. Utamaduni wa chama kimoja ni utamaduni hodhi na wa kiimla. Uongozi katika utamaduni wa chama kimoja unapatikana kwa njia za uteule, ukiwahusisha watu wachache wateule. Utamaduni wa chama kimoja unakataa ushindani wa wazi. Katika utamaduni wa chama kimoja kutamani cheo fulani ndani ya chama na katika serikali ni ulafi na uroho wa madaraka. Ndio maana vyama vyetu vyote vikubwa hapa nchini vinakataza na kukemea wanachama wao kutamani na kutangaza nia ya kuwania madaraka makubwa kama vile urais au uenyeviti wa vyama.

Kutamani madaraka peke yake kunakatazwa, achilia mbali kuandaa mkakati wa kushinda nafasi unayoitamani. Na hili ndilo kosa tulilolifanya. Tulikuwa wajinga sana kudhani kwamba tupo katika mfumo na utamaduni wa vyama vingi ambapo mtu yupo huru kutamani cheo chochote katika chama chake cha siasa, na kutengeneza mikakati ya kushinda cheo hicho katika uchaguzi huru ndani ya chama. Tulikuwa wajinga kwa kujaribu kuachana na utamaduni wa kuvizia cheo na kujifanya hutaki wakati unataka.

'Msaliti' mwenzetu Zitto Kabwe alianza siku nyingi mwaka 2009 kwa uamuzi wake wa kugombea uenyekiti wa chama bila kupata ridhaa ya wazee wa chama. Alikuwa mjinga kudhani kwamba uongozi katika mfumo wa chama kimoja unapatikana kwa kujaza fomu na kuomba kura. Nami nilikuwa mjinga nisiyeelewa kwa kumuunga mkono na kumtaka asonge mbele katika nia yake hiyo. Hakuishia hapo, Zitto Kabwe akafanya ujinga mwingine kwa kutamani na hatimaye kutangaza kugombea urais kupitia chama chake. Huu nao ulikuwa ni usaliti kwa utamaduni wetu wa chama kimoja, kwa sababu katika utamaduni huu nafasi kama hii ni ya kiteule na wateule na wateuaji wapo.

Ninapokubali kupokea lawama katika kushiriki kusababisha mgogoro unaoendelea ndani ya CHADEMA, naomba nami niwarushie lawama tele wanachama na mashabiki wa chama hiki, na wapenda mabadiliko kwa ujumla. Nawarushia lawama wanachama na washabiki wa CHADEMA kwa kuwashabikia viongozi wa chama chao katika kukinyonga chama. Viongozi wa chama hiki wamefanya makosa mengi na makubwa hadi kusababisha mgogoro ufike ulipofika, lakini wanachama na mashabiki wa chama wamekuwa wakishwashangilia katika kila hatua walioifanya. Kwa hiyo lawama ya kwanza kwa wanachama na mashabiki ni pale walipokubali kugeuzwa kuwa mashabiki wa viongozi ndani ya chama badala ya kuwa mashabiki wa chama. Na kwa kuwa ushabiki hupofusha macho na akili, mashabiki wa viongozi hawatofautishi kati ya uongozi na chama. Ni kama vile wamedanganywa na viongozi waliopo na wakakubali kudanganyika, kwamba uongozi wa chama ndio chama, na chama ndio uongozi!

Ni kwa sababu ya ushabiki kwa viongozi, ndio maana ilifika mahala wanachama na mashabiki wa CHADEMA wakagawanyika katika makundi ya washabikia viongozi, na chama kikakosa watu wa kukishabikia na hapo kikajikuta hakina mlinzi.

Makosa yaliyofanywa na uongozi na wanachama wa CHADEMA unafanana sana na makosa yaliyofanywa na viongozi na wanachama wa NCCR Mageuzi miaka ya tisini. Kama inavyotokea kwa CHADEMA leo, wanachama wa NCCR Mageuzi waligeuka kuwa mashabiki wa viongozi, kundi moja likimshabikia Mrema na kundi jingine likiwashabikia akina Marando. Kwa kudhani kwamba chama kilikuwa imara sana, kundi la akina Marando likaamua kumfukuza Mrema likiamini kwamba alikuwa hana madhara yoyote kwa sababu chama kilishaimarika mno, wakisahau kwamba msingi wa ufuasi ulijengwa kwa viongozi na sio kwa chama.

Mrema alipotimka, akatimka na mashabiki wake. Hicho ndicho kinachoendelea ndani ya CHADEMA. Kuna watu wenye mtazamo finyu wanaamini kwamba chama hiki ni imara sana kwa sasa kiasi kwamba hata wakimfukuza Zitto kitaendelea kubaki imara. Wamesahau kwamba wamejenga ufuasi kwa viongozi, na hivyo watakapomfukuza Zitto atatimka na wafuasi wake na chama kitayumba. Wangekuwa na mtazamo mpana wa kimantiki, na kama wangekuwa ni watu wa kujifunza, viongozi wa CHADEMA wangelimaliza sakata la Zitto ambalo sasa lipo mahakamani kwa njia ya usuluhishi kimya kimya kama walivyofanya NCCR kwa Kafulila. Lakini kwa sababu ya upofu unaoendelea unaotokana na kugubikwa na ulevi wa utamaduni wa chama kimoja kwa upande mmoja, na ulevi wa umaarufu kwa upande mwingine, hawatakubali yaishe nje ya Mahakama, na hatimaye watamfukuza Zitto. Wakishakumfukuza Zitto atatimka na mashabiki wake, chama kitayumba na kutoa unafuu kwa CCM. Katika mazingira haya tunahitaji sana mbadala wa CCM na CHADEMA.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments