[wanabidii] Kifo cha Mkuu wa UwT Rwanda na maisha ya ‘roho mkononi’ kwa ma-spy ‘wastaafu’

Monday, January 20, 2014
Moja ya matukio makubwa ya kiusalama mara baada ya kuanza kwa mwaka huu 2014 ni kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Rwanda, Patrick Karegeya. Mwili wa shushushu huyo wa zamani ulikutwa chumbani katika hoteli moja ya kifahari nchini Afrika Kusini (ambako Karegeya alikuwa akiishi kama mkimbizi) ukiashiria kuwa amenyongwa.

Mara tu baada ya kupatikana kwa taarifa hizo, lawama zikaanza kuelekezwa kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambaye japo aliwahi kuwa swahiba na Karegeya, wawili hao walitokea kuwa mahasimu wakubwa, hasa baada ya shushushu huyo kufungwa, kuvuliwa cheo chake cha Ukanali jeshini, n hatimaye kukimbilia mafichoni Afrika Kusini.

Kimsingi, kilichomkumba Karegeya kinaweza kumkumba shushushu yeyote yule pindi 'akipishana njia' (kutofautiana) na 
watawala. Kwa vile ushushushu ni taaluma inayohusika na masuala ya 'siri kuu' (top secrets), pindi shushushu akiwa nje ya ulingo kunajengeka hisia (za kweli au za kufikirika) kuwa ni mtu hatari anayestahili kudhibitiwa kwa gharama yoyote ile.

Lakini si katika suala la 'roho mkononi' katika maisha ya shushushu sio tu 'anapotibuana' na mwajiri wake au watawala bali pia hata wakati akiwa katika ajira lakini akikamatwa nje ya nchi, kwa mfano. Unless shushushu huyo ana umuhimu mkubwa kwa taifa husika, kanuni ya kawaida ni kwa taasisi yake na hata nchi husika kumkana kuwa hawamtambui. 

Na hata ndani ya nchi, ikitokea shushushu 'ameumbuka' (lugha ya kishushushu inayomaanisha 'kificho cha utambulisho' au 'kifuniko' au cover kwa Kiingereza) basi si ajabu kwa mwajiri wake kumkana hadharani hata kama kukumbuka huko si kwa makusudi. Hata hivyo, mazingira ya ndani ya nchi ni rahisi kwa taasisi ya ushushushu katika nchi husika kuyadhibiti, na hivyo kupelekea kutokuwa na ulazima wa kumkana mwajiriwa wake.

Tukirejea kwa tukio la mauaji ya Karegeya, baadhi ya wachambuzi wa mambo ya intelijensia wanabainisha kuwa kifo chake kilikuwa ni suala la lini kingetokea, na si kama iwapo kingeweza kutokea. Hisia hizo zinatokana na ukweli kwamba Karegeya alikuwa akifahamu mambo mengi kumhusu swahiba wake wa zamani Kagame. Na kwa kuendelea kwake kuwa 'huru' (au hai) kulikuwa ni tishio lililopaswa kumalizwa, kwa gharama yoyote ile.

Inaelezwa kuwa kabla ya kifo chake, shushushu huyo alifanya mahojiano na chombo kimoja cha habari na kutamka bayana kuwa yupo radhi kuwa shahidi dhidi ya Rais Kagame iwapo jumuiya ya kimataifa ikipanua uchunguzi kuhusu chanzo cha mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda kati ya mwaka 1994 na 1995. Inadaiwa kuwa Karegeya alieleza kwamba Kagame alishiriki moja kwa moja kuitungua ndege iliyombeba aliyekuwa Rais wa nchi hiyo kabla ya mauaji ya kimbari, Juvenal Habyarimana.

Licha ya mahojiano hayo, Karegeya alikuwa mmoja ya washiriki wa zamani wa Kagame (waliogeuka kuwa maadui wakubwa) ambao wapo mafichoni katika nchi mbalimbali duniani, hususan Afrika Kusini ambapo wanajishughulisha na harakati za kisiasa kumng'oa Kagame. Kadhalika, Karegeya na wenzake walijitokeza kuwa wakosoaji wakuu wa utawala wa Kagame, huku wakishinikiza jumuiya ya kimataifa kumbana kiongozi huyo katika masuala ya haki za binadamu nchini Rwanda.

Pengine kwa bahati mbaya au makusudi, kifo cha Karegeya kilitokea siku chache tu kabla ya maadhimisho ya miaka 20 ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda. Na katika maadhimisho hayo, Kagame alinukuliwa akitoa onyo kali kwa aliowaita 'wasaliti wa Rwanda' na kuahidi kuwa "ni suala la muda tu, yeyote aliyesaliti taifa letu lazima akumbane na madhara ya usaliti huo."

Awali, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo, Jenerali James Kabarebe, alikebehi kifo cha Karegeya na kudai "ukiishi kama mbwa utakufa kama mbwa, na wafagizi watautupa mzoga wako kutokana na harufu mbaya.

Pia, siku chache zilizopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo, alitetea uamuzi wa serikali ya Kagame kutohuzunishwa na kifo cha Karegeya, akidai kuwa shushushu huyo alikuwa 'adui aliyejitengeneza mwenyewe (self-declared enemy) dhidi ya Rwanda'

Kwa upande mwingine, kifo cha Karegeya ni mlolongo wa vifo mbalimbali vya 'wapinzani wa Kagame' wanaoishi ufichoni, ambapo takriban vyote vilivyotokea katika mazingira ya kutia shaka na lawama zikaelekezwa kwa kiongozi huyo wa Rwanda anayetuhumiwa na wapinzani wake kuwa ni dikteta anayotumia huruma ya nchi za Magharibi (kutokana na mauaji ya kimbari) kukandamiza upinzani na haki za binadamu nchini humo.

Na kwa hakika, Rais Kagame ni kipenzi cha viongozi wengi wa mataifa makubwa ya Magharibi. Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton anamtaja Kagame kama mmoja ya viongozi wachache mfano wa kuigwa barani Afrika, huku Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza akiwa na uhusiano wa karibu na kiongozi huyo wa Rwanda.

Ukweli kwamba chini ya uongozi wa Kagame, nchi yake imepiga hatua kubwa kiuchumi, na inatajwa kama moja ya nchi chache zenye uchumi unaokua kwa kasi duniani, unatajwa kuwa moja ya sababu kubwa ya nchi za Magharibi kufumbia macho kile kinachoelezwa kuwa ni udikteta na ukiukwaji mkubwa wa haki za kibinadamu nchini humo.

Nihitimishe makala hii kwa kutahadharisha kuwa hatma ya Rwanda inategemea sana jitihada za kujenga umoja wa kitaifa na kufuta makovu yaliyotokana na mauaji ya kimbari. Historia imeonyesha mara kadhaa kuwa tawala zinazotumia 'mkono wa chuma' hufanikiwa kuwa madarakani kwa muda mrefu lakini hatimaye huanguka. 

Mwanaharakati wa haki za watu Weusi huko Marekani, Dkt Martin Luther King, Jr aliusia kuwa "violence begets violence... We must meet the forces of hate with the power of love... Through violence you may murder the hater, but you do not murder hate. In fact, violence merely increases hate" (vurugu huzaa vurugu...ni lazima tupambane na nguvu za chuki kwa kutumia upendo...Japo kwa kutumia vurugu unaweza kumuua adui, lakini huwezi kuua chuki. Na kwa hakika vurugu huongeza tu chuki

---
Mwandishi: Chahali
Makala ya Raia Tanzania, toleo la Januari 16, 2014
Barua pepe chahali@about.me Blogu www.chahali.com 

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

0 Comments