[wanabidii] PUMZIKA BABA SENGODO MVUNGI

Tuesday, November 12, 2013
LALA BABA, SENGODO MVUNGU
 
Si rahisi kuamini, lakini umeshatutoka,
Sengodo mwana Mvungi, huzuni kutuachia,
Shambulio la mapanga, ubongo `kuutawanya',
Nenda Baba nenda, taifa lanyong'onyea.
 
Kwa matendo ya kihuni, uhuni ukafanyiwa,
Hofu kutanda nchini, hakuna aliye salama,
 Usokuwa na makuu, Mvungi kuhujumiwa,
Acha machozi yatoke, Mvungi umetutoka!
 
Sitazami ya kikale, vina kuvipangilia,
Chochote chenye huzuni, hapa ninakulilia,
Miongoni mwa walo bora, Mvungi ulitumika,
Pumzika kwa amani, Mwenyezi atakujazi.
 
Hukujawa na tamaa, za kupora na kuiba,
Mema kuyasimamia, kasoro kututajia,
Taaluma kueneza, vijana wakafaulu,
Kwa mapigo ya mapanga, uhai umekutoka!
 
Umelala chini chali, pumzi imekukatika,
Huko sote tutafika, lakini twahuzunika,
Chanzo cha kifo hakika, ndicho cha kuhuzunisha,
Wametenda walotenda, Mwenyezi akiwatazama.
 
Uchungu uloupata, dhahiri utawarejea,
Hata kama sio wao, bali wa kizazi chao,
Watakuswa kwa mwilini, hadi kwa mioyo yao,
Mwenyezi atasimama, maombi kuyasikiliza.
 
Yapo mengi ya kuyataja, Mvungi ulotutendea,
Kwa taifa na jamii, ni chanzo kukukumbuka,
Twazililia na nafsi, walokutesa, kukuua,
Hasira za Mungu wetu, zijibu maombi yetu.
 
Sasa tunaomboleza, hapa nukta niiweke,
Vidoleni kumetweta, jasho na kutetemeka,
Kuamini umekufa, Mvungi yataka moyo.
Pumzika Baba yetu, pumzika kwa amani.
 
Mashaka Bonifas Mgeta,
Dar es Salaam.
CELL: 0754691540
EMAIL: mgeta2000@yahoo.com
Tanzania.
 

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments