Ndugu Mhariri,
Nakuandikia Mtazamo wangu kufuatia Maoni ya Mhariri ya Gazeti lako la Mwananchi la tarehe 10 September 2013 yaliyokuwa chini ya kichwa cha habari "USAJILI WA MELI ZA KIGENI UANGALIWE UPYA" nikiamini kuwa utazingatia Maadili na Uweledi wa Tasnia ya Habari yanayotoa uhuru kwa wengine kutoa maoni yao na hivyo hutosita kuyachapisha Maoni yangu haya.
Kwa yeyote ambaye amesoma Maoni yale atakubaliana nami kuwa taswira anayopata ni kuwa yameandikwa na mtu aliyejawa na hasira na chuki dhidi ya Zanzibar. Lakini kwa Msomaji makini aliye na uchambuzi itamsikitisha kuwa hasira na chuki zile hazina msingi wowote zaidi ya husda ya kibinaadam.
Maoni yako yalifuatia tukio la kukamatwa kwa Meli ya mizigo ya Gold Star karibu na pwani ya Italy ikiwa na tani 30 za bangi. Meli hiyo imesajiliwa na Serikali ya Zanzibar kupitia Wakala wake aliyepo Dubai. Na hili likatosha kuamsha hasira za Mhariri.
Umelalamikia kuwa " jina la Tanzania limezidi kuchafuliwa mbele ya jumuiya ya kimataifa baada ya meli ya mizigo iliyosajiliwa Zanzibar kukamatwa ikiwa na tani 30 za bangi" Hivi kitendo cha kusajili chombo cha usafiri iwe cha baharini, angani au hata nchi kavu na baadae chombo hicho kikajiingiza katika vitendo vya uhalifu usiohusiana na usajili, lawama hurejea kwa Mamlaka iliyosajili chombo hicho? Kama hivyo ndio sahihi maana yake ni kuwa magari yote yanayohusika na uhalifu wa aina yoyote SUMATRA ilaumiwe kwa kutoa usajili kwa magari hayo!!! Na kila uchao magari hayo ndio wasafirishaji wakubwa wa Meno ya Tembo, madawa ya kulevya, wasafiri haramu mpaka wengine hufia ndani ya magari. Kama katika Usajili hakuna kosa, ni wazi uhalifu wa kawaida ulio nje ya uwezo wa Mamlaka inayosajili chombo hauwezi kumrudia na kumtia lawamani Msajili.
Kama ikichukuliwa hoja yako kuwa ni sahihi maana yake ni kuwa hata Viwanja vya Ndege vya Tanzania ambavyo vimekithiri kwa kutumiwa na wasifirishaji madawa ya kulevya navyo Lawama ielekezwe kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege. Maana hili sio siri kuwa Watanzania walioondokea Viwanja vya Ndege hivyo vya Tanzania wamejaa katika Magereza ya Nje na walisafiri kwa madege yalioruhusiwa na Mamlaka za Tanzania. Siamini kuwa huelewi kuwa wapekuzi katika Viwanja vya ndege vya nje huwa makini zaidi pale ndege inayotokea Tanzania inapotua kwa sababu ya kukithiri uingizwaji wa madawa ya kulevya kutokea Tanzania. Hivi sasa ni usumbufu ulioje kwa wote wenye Passport za Tanzania wanaposafiri kwenda nje.
Hata kilio cha Wazanzibari kudai Uraia utolewe katika Mambo ya Muungano ili kila mmoja awe na Hati yake ya kusafiria si kwamba hawana sababu!!! Leo Watanzania wote hupekuliwa kupitilia kwa vile hio ndio sifa tuliojijengea. Anasumbuka aliemo na asiyekuwemo. Kwa hoja yako vile vile hata Mamlaka inayotoa Hati za Kusafiria Tanzania nayo ibebeshwe lawama kwa kuwapa Hati hao Watanzania waliojaa magerezani kwa uhalifu hasa wa madawa ya kulevya. Maana hii nayo si aibu ndogo!!! Sio tu kuwa chombo kimesajiliwa Zanzibar, bali hawa ni Watanzania na wamepewa Hati halali za kusafiria.
Umeandika: "Tunashindwa kupata maneno stahiki ya kulaani kitendo cha kusajili meli za kigeni kiholela na kuziwezesha kufanya biashara au vitendo vya kihalifu, huku zikipeperusha bendera ya Tanzania. Hakuna ubishi kwamba usajili holela wa meli za kigeni ambao umekuwa ukifanywa na Serikali ya Zanzibar, sio tu umeharibu jina zuri la taifa letu mbele ya jumuiya ya kimataif…"
Inasikitisha kuwa hukutuonesha ushahidi wowote juu ya huo "usajili holela". Lakini ni kwa nini tumekuwa waoga sana wa kuharibu jina letu kimataifa bila kujali dhamira na silka zetu kuwa uovu ni uovu tu. Na tukaumia kuwa uovu husika umeathiri dhamira yetu, heshima yetu kwa jamii yetu humu humu ndani!!! Inasikitisha sasa tumeelekeza zaidi fikra zetu juu ya vipi hao "WA NJE" wanatuona sisi!!!! Lakini hatujali humu ndani tukoje!!!
Umekoleza sana kuwa Meli hiyo ikipeperusha bendera ya Tanzania kama vile umesahau kuwa bendera hiyo ni mali ya Shirka nusu kwa nusu kati ya Tanganyika na Zanzibar , isiwe nongwa Zanzibar kuipeperusha kwa mambo yake iliyo na Mamlaka nayo. Lakini hivi ni kweli hilo "jina zuri la taifa letu" huko nje limeharibiwa na huo Usajili??? Nchi inayoongoza kwa mauaji ya Albino duniani (ambapo takriban mia wameuliwa) pasi hatia yoyote mbali waliokatwa viungo kinyama, mauaji ya vikongwe yaliokithiri, ukeketaji, rushwa iliokomaa, usafirishaji wa madawa ya kulevya, ujambazi wa kutisha wa kutumia silaha- na haya yote unayajua yanatokea upande gani wa Jamhuri hii yenye "jina zuri".
Amma kweli nyani haoni lake. Nikukumbushe tu hata Zanzibar sasa inaongoza kwa uhalifu wa matumizi ya silaha wakati Znz ni marufuku kumiliki silaha. Ukichunguza wahusika utagundua zimetokea wapi. Na huko zinakotokea ziko Mamlaka zinazosajili na kuruhusu umiliki wa silaha – jambo ambalo ni nyeti sana. Lakini Mamlaka hii iko T/Bara na hivyo hailaumiliki.!!!
Umeandika:" Yafaa tujikumbushe hapa, angalao kwa muhtasari tu jinsi usajili huo holela ulivyosababisha maafa na kuharibu jina la taifa letu nchi za nje. Bila shaka sote tunakumbuka maafa yaliyotokea huko Zanzibar kutokana na kuzama MV Spice Islander na MV Skaget ambapo watu wengi walipoteza maisha kutokana na ubovu wa meli hizo" Tudhibiti chuki zetu zisitufanye vipofu na wapindishaji ukweli. Hakuna ukweli wowote kuwa Meli zile zilikuwa na ubovu wowote. Ripoti za Tume hazikueleza hilo. Kilichoelezwa kama chanzo cha ajali ya MV Spice na MV Skagit ni uzidishaji mizigo na abiria na baadhi ya uzembe.
Sisi ilituuma kupoteza ndugu zetu. Na inatuuma hadi leo. Na inatukera kutumia maafa yale kutuongezea lawama eti "tumeharibu jina letu nchi za nje" Kwani hivi maafa ya MV Bukoba nayo si itakuwa yaliharibu jina au kwa vile aliesajili ni Tanzania Bara? Maana hii ndio ajali ya mwanzo kubwa kwa Tanzania iliogonga medani za kimataifa.Kama maafa yanaharibu jina kimataifa jee unajua kuwa Takwimu zinaonesha kila mwaka Tanzania Bara zaidi ya watu elfu tano hufa kwa ajali za barabarani tu???!!! Hao ni mbali na wanaoathirika na kubaki vilema ambao inasemekana (tena kitakwimu) kuwa hawa ni wengi kuliko wanaozaliwa. Jee huko hakuna Mamlaka inayosajili vyombo hivyo?
Mwisho ulimalizia kwa kuandika:" Tunadhani sasa umefika wakati wa suala la usajili wa meli za kigeni kuwa suala la Muungano" Hapa unajenga dhana kuwa Zanzibar haiwezi kusimamia mambo yake na kila itokeapo changamoto yoyote ( hata ya uzushi kama hii ambayo Znz haina lawama yoyote) basi suluhisho ni kuhamishia suala hilo Bara. Sijui hili tuliite vipi kama si dharau iliokithiri. Angalau ingekuwa huko Bara kuna utakatifu usio shaka pengine ungeeleweka. Lakini hivi hukuona njia nyengine zaidi ya hio? Unaonaje tukitafakari njia ambayo inaweza kufanya kila mmoja akabeba lawama na aibu yake? Pengine wakati huo hata muelekeo wa vyombo vyenu vya habari utabadilika. Leo jambo ovu likitokea Znz hilo litakuzwa mpaka lipitilie lakini jambo hilo hilo litokee upande wa pili litapozwa tu. Hivi punde yametokea matukio ya matumizi ya tindikali dhidi ya binadamu. Ni matukio yanayostahiki kulaaniwa kwa nguvu zote. Lakini angalia mulivyoripoti yale ya Znz na yale ya T/bara. Hayafanani mbingu na ardhi.
Zanzibar akipigwa risasi mtu ingawa huku ni marufuku kumiliki silaha huo ni "UGAIDI ZANZIBAR" Lakini mfanyabiashara bilionea mwekezaji mzalendo katika sekta ya madini wa Arusha aliyemiminiwa risasi kinyama huo ni uhalifu. Mfanyabiashara mwekezaji mzalendo bilionea wa Dar alipomwagiwa tindikali huo ni uhalifu tu. Mabomu yanaporipuliwa mikutanoni Arusha huo ni uhalifu tu. Si ugaidi wala hauharibu jina zuri la taifa letu. Ama kweli akutukanaye hakuchagulii tusi.
AHSANTE SANA.
Said, A. Ali
Zanzibar
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
0 Comments