[wanabidii] Tusitishe utoaji leseni za gesi na mafuta mpaka sera na sheria ikamilike

Thursday, September 19, 2013

RAIS ASITISHE MZUNGUKO WA NNE WA UTOAJI LESENI ZA UTAFUTAJI WA GESI ASILI NA MAFUTA MPAKA SERA NA SHERIA ZA GESI ASILI ZIKAMILIKE NA MAREKEBISHO YA SERA YA NISHATI NA SHERIA ZA MAFUTA YAFANYIKE.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais Jakaya Kikwete anapaswa kusitisha mzunguko wa nne wa utoaji wa leseni za utafutaji wa gesi asili na mafuta mpaka sera na sheria ya gesi asili zikamilike na marekebisho ya sera ya nishati na sheria za mafuta yafanyike kwa kurejea maoni na mapendekezo niliyoyawasilisha bungeni kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani tarehe 22 Mei 2013.

Rais anapaswa kuchukua hatua hiyo kwa kuzingatia kwamba tarehe 25 Mei 2013, badala ya kushughulikia mapendekezo hayo, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo alitoa majibu ya uongo na upotoshaji bungeni kuhusu masuala mbalimbali.

Aidha; Ikulu inapaswa kueleza iwapo Baraza la Mawaziri chini ya Rais Kikwete ndilo lililofanya  uamuzi wa kuendelea na mchakato wa kutoa leseni za vitalu vya utafutaji wa gesi asili bila ya kuwepo kwa sera ya gesi asili na sheria ya gesi asili na
 huku sera ya nishati na sheria zinazohusu mafuta au ni maamuzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na Wizara ya Nishati na Madini.

Kwa upande mwingine; Waziri Mkuu Mizengo Pinda anapaswa kueleza iwapo  kauli ya kejeli, dharau na uongo ya hivi karibuni iliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospter Muhongo kwamba  uwezo wa wafanyabiashara wa Tanzania ni kuwekeza kwenye soda na juisi, si kwenye sekta ya gesi; ni msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au maoni yake binafsi.

Izingatiwe kwamba  Wizara ya Nishati na Madini, kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), imetanganza mzunguko wa nne wa utoaji leseni za utafiti wa gesi asilia na mafuta katika vitalu 8 ndani na nje ya maji ya Ziwa Tanganyika vyenye ukubwa wa Kilomita za mraba elfu tatu kila kimoja utakayofanyika Oktoba 2013.

Serikali pia, imetenga mipaka ya vitalu 2 kwenye bahari kuu, kuingia na ubia wa utafiti na kampuni inayoitwa mbia wa kimkakati (Strategic Partner) ambae serikali haijamtaja.

Mchakato huu unafanyika wakati taifa likiwa halina sera (mchakato wa kuiandika bado unaendelea) na hatimaye yaanze maandalizi ya kupata  sheria mahususi za kusimamia sekta ndogo ya gesi hatua ambayo inapaswa kuambatana na marekebisho ya kisera na kisheria ya sekta . 

Ikumbukwe kwamba tayari Tanzania imeshafanya ugunduzi wa futi za ujazo zaidi ya trilioni 32 za gesi katika maeneo kadhaa nchini, nchi kavu na baharini, ambazo unaifanya Tanzania kuwa kati ya nchi vinara kwa gesi nyingi Afrika na duniani. 

Utajiri huu wa gesi hadi sasa hauna sera wala sheria zinazotoa mwongozo wa usimamizi na udhibiti wake, ili kuhakikisha unawanufaisha Watanzania, kuepuka makosa yaliyofanyika katika uwekezaji mwingine wa gesi asili na rasilimali nyingine uliofanyika bila mifumo thabiti. 

Matokeo ya kuwepo kwa ombwe la kisera na kisheria ni madhara yanayojitokeza  sasa ya kukosekana au kupuuzwa kwa ushiriki stahili wa wananchi wa kada zote, hali ambayo imesbabisha vurugu na hata kusababisha umwagwaji wa damu za raia wasiokuwa na hatia huko maeneo ya  Mkoa wa Mtwara na migogoro katika mkoa wa Lindi. Hadi sasa tunavyozungumza, wananchi hao wanendelea kuishi katika hali ya hatari isiyotangazwa rasmi rasmi.

Wakati Watanzania wa ngazi za chini, mfano hai wakiwa hao wa maeneo ya Mtwara na Lindi, wakifanyiwa unyanyasaji na ukatili dhidi ya ubinadamu kwa sababu tu wanadai uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali zinazotapanywa na viongozi wao walioko madarakani, wananchi wa ngazi ya juu na jumuiya za wafanyabiashara wazawa, wakubwa na wadogo, halikadhalika hawajatengenezewa mazingira mazuri ya kushiriki katika sekta hiyo kwa maana ya uwekezaji. 

Msimamo wa Wizara ya Nishati na Madini siku zote umekuwa ni kwamba, ushiriki pekee wa wazawa katika sekta hii ni kuwauzia bidhaa kwa ajili ya matumizi (consumable goods) makampuni ya kigeni yaliyowekeza kwenye utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi nchini. 

Ni msimamo wangu kwamba kusema eti ushiriki pekee wa wazawa ni katika kuuza consumable goods ni kuwadhalilisha na kuwatukana wawekezaji wa ndani, na kudhihirisha kwamba Serikali ya CCM kupitia Wizara ya Nishati na Madini haina wala haijawahi kuwa na dhamira ya kustawisha wawekezaji wazawa, kwa ajili ya kunufaisha nchi nzima na Watanzania wote.

Katika mtindo wa sasa ambapo Serikali inaingia katika Mikataba ya utafutaji na uzalishaji  wa pamoja wa mafuta na gesi maarufu kama Production Sharing Agreements (PSA) ni makampuni machache ya Kitanzania yanayoweza kuingia katika mikataba hiyo na TPDC; bila marekebisho ya kimfumo wa ushiriki na uwezeshaji kupitia sera, sheria na njia zingine.

Jambo la muhimu ni kwamba PSA sio mtindo pekee ya kibiashara katika utafutaji wa gesi; mitindo mingine ya kiutafiti ni pamoja na unaojulikana kitaalamu kama Farm In, Farm Out Agreements na Joint Operating Agreements (JOA).

Kwenye Farm In/Farm Out Agreements, Kampuni ambayo si mmiliki wa leseni ya utafiti au uendelezaji mafuta na gesi inaweza kununua hisa  (au kutoa mchango wa kimaslahi) kwenye kampuni ambayo tayari inayo leseni ya utafutaji, na hivyo kampuni zote kupata faida kutokana na ugunduzi na uuzaji wa gesi au mafuta; uwepo wa sera na sheria utaweza kushughulikia suala hili. 

Mtindo Joint Operating Agreements (JOA) makampuni yanaingia ubia wa kufanya shughuli za uchimbaji wa pamoja kwenye makubaliano ya Ubia wa Pamoja (Joint Venture), ambapo hatari za kiuwekezaji zinapunguzwa na gharama kubwa za utafiti na utafutaji zinabebwa kwa pamoja; hii inaweza kuwekewa mfumo wa utekelezaji kupitia sera na sheria.

Hivyo kitendo cha Waziri Muhongo na Serikali ya CCM kuona kwamba hakuna namna ya wazawa kushiriki ni kutokana na udhaifu wa kisera na kisheria ambao athari zake huongezeka zaidi panapokuwepo na ufisadi na uongozi mbovu; hivyo, iwapo Serikali haitatoa kauli ya kusitisha au kuahirisha mchakato wa utoaji wa leseni hizo za utafutaji nitaeleza hatua ambazo tutachukua.

Imetolewa na John J. Mnyika (Mb)

Waziri Kivuli, Wizara ya Nishati na Madini

19 Septemba, 2013


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

0 Comments