[wanabidii] 'Taja jina la bibi mzaa mama wa Yesu Kristu!'

Friday, September 27, 2013
RAI, Alhamisi, Septemba 26, 2013; Na Joe Beda


MIAKA zaidi ya 10 iliyopita nilisoma katuni moja kwenye gazeti la SANI ambayo huenda ndiyo katuni yangu bora niliyowahi kuiona kwani ilinifikirisha na kunichekesha kuliko nyingine nyingi. Kipindi hicho kulikuwa na vuguvugu kubwa la haki za mtoto na hasa mtoto wa kike, huku kukiwa na wimbi la walimu kadhaa wa kiume kushitakiwa mahakamani kwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi wa kike.

Sijui kama suala hilo kwa sasa limekwisha, limepungua au limeacha kuripotiwa kwa sababu ya kupitwa na wakati, lakini inavyoonekana hali kwa sasa si sawa na kipindi kile.

Katuni ile ilimwonyesha mtoto wa kike akiwa amelala chini huku mwalimu wa kiume akimtandika bakora mfululizo na kumuuliza swali hili: "Nakuuliza, Tanganyika ilipata Uhuru tarehe 9 Desemba mwaka 1961, ilikuwa juma ngapi?"

Mchoraji wa katuni ile aliiwekea maandishi ya utangulizi yaliyosemeka; 'ukiona mwalimu anauliza swali hili, ujue ana lake jambo!' Hakika lilikuwapo jambo kati ya binti huyo, mwalimu, na swali lile la 'kizushi'.

Naam, nilicheka. Lakini nikajiuliza iwapo swali hilo ningeulizwa mimi ningekuwa na jibu? Tarehe ya Uhuru wa Tanganyika na hata Uhuru wa nchi nyingine kadhaa za Afrika tumekuwa tukikaririshwa miaka nenda rudi, lakini siku haswa ya tukio! Hapana.

Kumbukumbu za katuni hiyo zikanirudia majuzi baada ya watu wanaoaminika kuwa ni magaidi (wana mgambo) wa kundi la Al-Shaabab kuvamia mlolongo wa maduka ya Westgate Mall jijini Nairobi.

Mashuhuda walionusurika kuuawa kwenye tukio hilo, wameviambia vyombo mbalimbali vya habari kwamba magaidi hao walikuwa wakijitahidi kuwatenganisha 'walengwa' wao na 'wenzao' kwa kuwauliza jina la mama wa Mtume Mohammad (SAW)!

Sina uhakika na ugumu au wepesi wa swali hilo kwa 'muumini' mzuri, lakini nilicho na uhakika nacho ni kwamba, hata swali jepesi kama 'jina lako nani' unaweza kushindwa kulijibu kwa wakati ukiwa umeelekezewa mtutu wa bunduki na mtu asiye na masihara hata kidogo!

Mtu aliyeamua kwamba siku hiyo ndiyo siku yake ya kufa, labda itokee bahati mbaya, ni mtu hatari sana. Fikiria, tayari umeshuhudia watu wanne au watano wakipigwa risasi mbele yako baada ya kuulizwa swali, inafika zamu yako na kuulizwa 'jina lako nani?' hakika unaweza kushindwa kujibu!

Nikafikiria hivi kuna 'waamini' wenzangu wangapi wanaoweza kuulizwa ghafla na kutaja jina la bibi yake na Yesu mzaa mama? Tena hilo linaweza kuwa jepesi, lakini ni nani analijua jina la bibi yake Yesu mzaa baba mlezi?

Kwa kumbukumbu za haraka, nikakumbuka jina la Anna (Mtakatifu Anna) kuwa ndilo jina la mama yake Bikira Maria (bibi yake Yesu upande wa mama), lakini upande wa baba mlezi! Hatari.

Sasa hapo hakukuwa na shinikizo lolote, je ningekuwa nimeelekezewa bunduki? Hakika nikaikumbuka ile katuni kwamba ukiona mtu anauliza swali kwa mtindo huo, ujue ana lake jambo.

Nikawaza kuwa kama ingetokea bahati mbaya nikawa mmoja wa waathirika wa tukio la Nairobi, swali la haraka ambalo ningewajibu jamaa wale bila kusita ni kama wangeniuliza jina la mke (mkubwa) wa Mtume (SAW).

Haya mambo nikuomba Mungu yasikutokee. Ni mambo ya kusikitisha sana na hata kwa fikra za kawaida unashindwa kuelewa chuki hizi zinapandikizwa miongoni mwa binadamu kwa lengo gani?

Swali gumu zaidi ni jinsi gani ya kuzuia matukio ya kishenzi kama haya kutokea katika dunia hii ya utandawazi.

Jeshi la Polisi nchini limesema kwamba liko tayari, eti limejiandaa kuyakabili matukio kama haya; ni jambo la kushukuru kama kweli tuko tayari, lakini kikubwa ni kuyakinga yasitokee.

Ni hapo ndipo Watanzania wote tunapaswa kushirikiana. Ulinzi na usalama wetu unaanzia kwetu wenyewe, kwa kutoa taarifa kwa viongozi kuhusu mienendo ya kutia shaka ya kundi la watu au mtu yeyote unayemfahamu au usiyemfahamu.

Ipo tabia yetu ya kutowaamini watendaji kadhaa serikalini kwamba unaweza kutoa taarifa, kumbe unayemtaarifu anahusika au kuhusiana na kundi hilo matokeo yake usalama wako ukawa hatarini.

Sasa ushauri wangu katika jambo hilo ni kwamba, mtafute kiongozi unayemwamini hata wa chama cha upinzani, mtaarifu suala hilo na ninaamini yeye hataogopa kulipeleka serikalini; au basi mdokezee mwandishi wa habari unayemwamini kwani nao katika tasnia yao ni 'risk takers'.

Lakini serikali nayo inapaswa kuwa makini. Iweke mtandao mpana wa kugundua uingizwaji nchini wa 'fedha chafu' au hata kama ni safi, lakini zinapoingizwa kwa wingi kwa kundi au mtu asiyeaminika, ni vyema zikazuiwa hadi itakapofahamika kazi ya fedha hizo nchini ni ipi hasa.

Ni wazi maandalizi ya shambulio kama hili la Nairobi yaligharimu fedha nyingi. Sasa. Fedha hizo ziliingizwaje nchini? Zilipitia benki gani? Zilikwenda kwa nani?

Tusiruhusu fedha chafu kufika mikononi mwa watu ambao mienendo yao inatia shaka.

Nimalizie kwa kuwakumbusha 'wazee' wenzangu muziki mmoja wa miaka ya 1970 uliokuwa na maneno 'wanyama wabaya maana yake, sio simba wala si tembo, ni wanadamu wenye choyo…'


Nawasilisha
0684 419 506

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

0 Comments