[wanabidii] Taasisi ya Hifadhi ya Bunge la Marekani yamtunuku Rais Kikwete

Saturday, September 21, 2013
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa Jumatano, Septemba 18, 2013, alitunukiwa heshima ya pekee duniani ya kupatiwa Tuzo ya Mhenga ya Taasisi ya Kimataifa ya Hifadhi ya Bunge la Marekani (ICCF) katika sherehe ya kufana ya Chakula cha Usiku iliyofanyika kwenye ukumbi maarufu wa Andrew Mellon mjini Washington, D.C.

Rais Kikwete ametunukiwa Tuzo la Mhenga ambayo ni Tuzo ya Mtunzaji Bora wa Hifadhi wa Mwaka wa ICCF kwa kutambua na kuheshimu mchango wake mkubwa na uliotukuka katika jitihada za Uongozi wake na wa Tanzania kuhifadhi wanyama, mbunga na maeneo ya hifadhi ya wanyama pamoja na mazingira.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Tuzo hiyo kutolewa kwa yoyote kwa jina la Mhenga (Neno la Kiswahili lenye maana ya Mtu 
wa Kale) na mamia kwa mamia ya watu wakubwa nchini Marekani, wakiwamo Maseneta, Wajumbe wa Bunge la Wawakilishi la Marekani, Wafanyabiashara Maarufu, Watunzaji Hifadhi hodari duniani na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) Mama Dkt. Nkosazana Dlamini Zuma walihudhuria sherehe hiyo ya kuvutia ya Chakula cha Jioni.

Baadhi ya watu maarufu waliozungumza ama kutoa Tuzo nyingine katika sherehe za Chakula hicho ambako walihudhuria wageni zaidi ya 500 na ambako washereheshaji walikuwa ni pamoja na aliyekuwa Balozi wa Marekani katika Tanzania Mheshimiwa Mark Green pamoja na Mbunge wa Bunge la Wawakilishi la Marekani, Mheshimiwa Allen Boyd ni pamoja na Seneta Lindsey Graham ambaye alizungumzia Sera za Misaada ya Nje ya Marekani.

Wengine waliozungumza ama kutoa Tuzo ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mama Hillary Clinton ambaye alizungumza kwa njia ya video, Mwakilishi Jim Moran, Mwakilishi Betty McCollum, Seneta Saxby Chambliss, Seneta Rob Portman na Mwakilishi Ed Royce.

ICCF ina nchi wanachama 46 duniani na 40 kati ya hizo ziliwakilishwa katika Sherehe hiyo ya aina yake ikiwamo Kenya kutoka Afrika, Jordan kutoka Mashariki ya Kati na Colombia kutoka Marekani Kusini.

Sherehe za mwaka huu za kutoa Tuzo za ICCF ambayo ndiyo taasisi maarufu zaidi katika Bunge la Marekani ikiwa na maseneta 31 kutoka vyama vyote vikuu vya Marekani vya Democrat na Republican, Gavana mmoja wa Jimbo Mheshimiwa Sam Brownback wa Jimbo la Kansas na chama cha Republican na Wabunge wa Baraza la Wawakilishi 128 ziliongozwa na kaulimbiu isemayo: "Hifadhi katika Afrika: Usalama, Demokrasia na Maendeleo".

Mwenyekiti wa Sherehe za mwaka huu za Tuzo za ICCF Dkt. Cristian Samper alikuwa ni Rais na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Wildlife Conservation Society ambaye amefuata katika nyayo za wenyeviti wengine wa shughuli hiyo waliopita ambao ni Marais wa zamani wa Marekani Bill Clinton na George Herbert Walker Bush, Malkia Noor wa Jordan, Waziri wa Fedha wa Marekani Mheshimiwa Hank Paulson, Mawaziri wa Mambo ya Ndani wa zamani wa Marekani Mheshimiwa Bruce Babbit na Mheshimiwa Dirk Kempthorne.

Na mbali na Rais Kikwete, wageni wengine maalum wa Sherehe za mwaka huu za Tuzo za ICCF walikuwa ni Mama Zuma, Mtawala Mkuu wa Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa ya Marekani Dkt. Rajiv Shah, na Dkt. Naoko Ishii, Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Global Environment Facility.

Mbali na Rais Kikwete, viongozi wengine waliopata kutunukiwa Tuzo ya juu ya ICCF ni Waziri Mkuu wa Uingereza Mheshimiwa Tony Blair, Rais wa zamani wa Mexico Mheshimiwa Felipe Calderon, Waziri Mkuu wa Norway Jens Stoltenberg na Prince Albert wa Pili wa Monaco.

Akimtambulisha na kumkaribisha Rais Kikwete kupokea Tuzo hiyo, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya ICCF, Mheshimiwa David Barron alimwelezea Rais Kikwete kuwa ni rafiki wa hifadhi, mtu ambaye ametoa mchango mkubwa katika kulinda hifadhi katika nchi Tanzania na katika Afrika.

"Hatuwezi kutumia upande usiofaa wa akili yetu kufikiria. Hakuna shaka kuwa Rais Kikwete ana ari kubwa ya hifadhi ya wanyama, ya mazingira na ya dunia yetu kwa jumla na amethibitisha ukweli huo. Ni rafiki mkubwa tuliyenaye katika Afrika. Naomba tumkaribishe usiku wa leo."

Akizungumza baada ya kuwa amepokea Tuzo la Mhenga, Rais Kikwete alisema kuwa shughuli za hifadhi katika Tanzania na Afrika zinakabiliwa na changamoto kuu tatu ambazo ni mgongano kati ya hifadhi ya wanyama na ongezeko la watu ambako watu wameongezeka na wanadai ardhi zaidi ya kilimo na kufanyia shughuli zao nyingine, na mgongano kati ya binadamu na wanyama kwa maana wanyama kuharibu mazao na mali za watu.

Rais Kikwete alisema kuwa changamoto ya tatu ni ujagili dhidi ya wanyama, ukataji haramu wa miti jambo ambalo "limefikia kiwango cha kutisha kabisa na lisilovumilika."

Hata hivyo, Rais Kikwete aliihakikishia dunia kuwa Tanzania itaendelea kulinda kwa njia zote, ikiwa ni pamoja na kutumia jeshi, mbuga za wanyama, hifadhi za wanyama na maeneo ya wanyama. Tanzania ina mbuga 17 za wanyamapori, maeneo ya hifadhi 28, maeneo 43 ya kulinda wanyamapori na maeneo 38 ya kuthibiti wanyamapori.
Tokea mwaka 1961 wakati wa Uhuru, Tanzania imetenga kiasi cha asilimia 30 ya eneo lake lote kwa ajili ya hifadhi ikiwa ni pamoja na hekta 12.5 milioni za misitu.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

19 Septemba, 2013

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

0 Comments