[Mabadiliko] Wanaopigwa wanapoongezeka, CCM haibaki salama

Sunday, September 08, 2013
Wanaopigwa wanapoongezeka, CCM haibaki salama

Na Mashaka Mgeta
8th September 2013

January, 27 2001, makumi ya Watanzania waishio kisiwani Pemba, walipigwa, miongoni mwao wakauawa, kujeruhiwa na wengine kuikimbia nchi. Wakawa wakimbizi na kuweka historia ya kwanza kwa Tanzania-kuzalisha wakimbizi.
Baada ya tukio hilo, vyombo vingi vya habari vilipoandika, viliwaainisha waathirika wa kadhia hiyo kama 'Wapemba'. Hata mauaji yenyewe yakaitwa 'mauaji ya Wapenda'.
Siku chache baada ya mauaji hayo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, alizungumza na waandishi wa habari mjini Chakechake, pamoja na mambo mengine, akakemea ubaguzi uliodhihirika katika kadhia hiyo.
Maalim Seif ambaye sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, akasema na kunukuliwa na vyombo vya habari kuwa, waliouawa, kujeruhiwa na kuwa wakimbizi, hawakupaswa kutajwa kuwa 'Wapemba', bali wakimbizi.
Akasema sababu na dhuluma zilizowafanya Watanzania waishio Pemba kuandamana hata kupigwa risasi, kuuawa, kujeruhiwa na kuikimbia nchi, zikidhihirika upande wa Tanzania Bara, hali itakuwa vivyo hivyo.
Akaiasa jamii (kwa wakati huo), kwamba ni lazima tukio la 'mauaji ya Pemba' lijadiliwe kwa mtazamo wa kitaifa, huku msingi wake ukiwa ni haki sawa kwa watu wote.
Ni takribani miaka 12 sasa tangu Maalim Seif, atoe karipio hilo, Tanzania Bara ikishuhudia machafuko, vipigo, mauaji na mateso ya aina nyingine.
Taifa linalojinasibu kwa misingi ya amani na utulivu, sasa `linanuka' vurugu, ubabe, matumizi mabaya ya vyombo vya dola hususani yaliyojikita katika 'piga, ua, garagaza'. Haipendezi!
Nimekumbuka karipio la Maalim Seif baada ya kuwapo mfululizo wa matukio yanayofanana, ama yenye matokeo kama yaliyotokea katika 'mauaji ya Pemba', yakifanyika Tanzania Bara.
Imekuwa kawaida kusikia raia wamepigwa virungu, wamesambaratishwa kwa mabomu ya machozi na pengine kupitia risasi za moto zinazosababisha vifo na majeraha!
Inapotokea hali hiyo, siasa zinaingizwa katikati yake, propaganda zinaenezwa ambapo 'wa huku' wanawalaumu 'wa kule'. Tumanini la kubaini na kupata vyanzo na namna ya kupata suluhu ya kudumu, linatoweka.
Lakini vyanzo vinajikita katika karipio la Maalim Seif, kwamba kama sababu zilizowafanya Watanzania waishio Pemba kujikuta wakipigwa, wakiuawa na wengine kuwa wakimbizi, zikibainika kwa Tanzania Bara, matukio kama ya Pemba, yataenea nchi nzima.
Kwa uhalisia wake, ni dhahiri kwamba kuna kitu kinahitajika kwa jamii, kisipatikane. Kuna mambo yasiyohitajika na yanayokera, yanatendwa kwa jamii licha ya ukweli kwamba hayahitajiki.
Watendewa katika hayo wanaguswa katika nafsi zao, wakati watendaji wanafumba macho yao, wasione na kuziba masikio ili wasisikie. Nchi inajikuta katika vurugu zinazoweza kuepukwa.
Mwishoni mwa wiki hii, jamii imeshuhudia kipigo kwa baadhi ya wabunge wa upinzani, kikitokea ndani ya Bunge. Askari wa ulinzi na usalama waliingia kuwadhibiti, ili kukidhi agizo la Naibu Spika, Job Ndugai.
Badala ya kusikiliza hoja zenye maslahi kwa nchi, umma ukashuhudia ngumi, mateke na wengine wakibebwa mzobe mzobe mithili ya vibaka wanaoibia abiria ndani ya daladala, ingawa nao hawaistahili adhabu hiyo!
Kipigo kwa wabunge wa upinzani bungeni kinarejea katika karipio la Maalim Seif, kwamba kama kilichowashinikiza Watanzania wa Pemba, kitatokea kwa namna yoyote upande wa Bara, hali itakuwa ile ile.
Kwa hili la bungeni, wabunge wa upinzani wamekosoa mchakato wa Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Katiba Mpya, msingi wake ukijikita katika kupanua wigo wa kuwashirikisha Wazanzibar.
Kwa maana hiyo, wabunge wa upinzani waliondoa maslahi yao binafsi katika hilo, maslahi ya majimbo yao ya uchaguzi, maslahi ya vyama vya siasa, wakajiweka katika ya maslahi mapana ya Zanzibar iliyo sehemu ya Tanzania.
Kama wabunge wa upinzani wangeegemea kwenye maslahi ya familia, majimbo ama vyama vyao, ni dhahiri kwamba umma ungewadharau, ungewapuuza na kuwaona hawana maana.
Lakini inapofikia kwa Mbunge kama Joseph Mbilinyi, kubebwa mzobe-mzobe, sababu ikiwa ni kutetea maslahi ya nchi yanayojikita katika kuwawezesha Wazanzibar kupata fursa sawa katika mchakato wa sheria hiyo, kuna haja gani ya kumdhalilisha?
Kama Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu, angekuwa anatetea maslahi ya rafiki yake wa kike, ndugu zake, rafiki zake kama Kabby na Jerry, ama ya Chadema hata kufikia `kupigwa mtama' na kuondolewa bungeni kwa aibu, angezomea kuanzia Dodoma hadi Mbeya Mjini.
Lakini chanzo cha kadhia hiyo ni haki sawa inayotakiwa kuwapo kwa Watanzania wote, hususani Wazanzibar pale hoja kuhusu sheria hiyo inapohusika.
Siamini kama kuna mmoja kati ya wabunge wa upinzani ama kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaopenda vurugu. Hata mimi siamini katika suluhu ya tatizo linaloelekezwa ama kupatikana kwa njia za vurugu.
Ila, inapotokea kuwapo ongezeko kubwa la raia pasipo kujali nyadhifa zao, kupigwa na askari wa ulinzi na usalama, wale wanaojumuishwa miongoni mwa vyombo vya dola vya serikali inayoundwa na CCM.
Kwa kadri raia wa kijijini anavyonyanyaswa na askari walio katika vituo vya polisi, wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga wanavyotendewa hivyo hivyo, wanakuwa katika kundi la wanyonge, wanaoteswa na vyombo vya dola.
Kadri wanafunzi hasa wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu `wanapopata kichapo cha polisi' wakiwa katika mgomo wenye lengo la kudai haki zao, kama ilivyo kwa wafanyakazi, wanakuwa katika kundi la wanyonge, wanaoteswa na vyombo vya dola.
Kadri wabunge wa upinzani wanapodhibitiwa kwa nguvu za askari wa ulinzi na usalama, wakapigwa makonzi, kofi, teke, ngumi na kuburuzwa mfano wa gunia lenye taka ngumu, kwa hoja zinazogusa maslahi ya walio wengi.
Wabunge hao wanakuwa katika kundi la wanyonge, wanaoteswa na vyombo vya dola.
Orodha hiyo inavyozidi kuongezeka, shutuma za dhahiri zikielekezwa kwa vyombo vya dola vilivyo chini ya serikali iliyoundwa na CCM, shutuma zinakuwa kwa CCM.
Kwa hali hiyo, kunaibuka kundi la wateswaji (walio wengi) na watesaji wanaoitegemea dola. Wateswaji wanajikuta kuwa ni raia wa kawaida, wanataaluma, wanafunzi, watumishi, wanasiasa hasa wawakilishi wa wananchi.
Hilo ni kundi kubwa ambalo linapojieneza Mashariki hadi Magharibi, Kaskazini hadi Kusini mwa nchi, CCM haiwezi ikabaki salama. Itayumba, itakosa mashiko kwa umma, itakimbiwa na kukataliwa katika chaguzi, hata kama ni kwa njia ya reja reja.
Kuliandika hili linaweza kuwafanya wahafidhina kuamini kwamba kunatokana na 'damu ya upinzani' inayojieneza kwa raia walio wengi, lakini si hivyo, bali uhalisia na ukweli wa historia ya mwanadamu.
Ndivyo ilivyo.
Mashaka Mgeta ni Mhariri wa Makala wa gazeti hili ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya siasa. Anapatikana kupitia simu namba +255 754 691540, +255716 635612 ama barua pepe: mgeta2000@yahoo.com.
 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI((http://www.ippmedia.com/frontend/index.php?l=59068)
 

Share this :

Related Posts

0 Comments