[wanabidii] Rasimu ya Katiba Mpya: Andiko kwa Taifa lisilosoma

Thursday, July 18, 2013
Ni takribani mwezi sasa toka rasimu ya katiba mpya izinduliwe. Rasimu ikiwa ni moja ya hatua muhimu katika mchakato wa katiba mpya baada ya wajumbe wa tume ya katiba kuzunguka kwa wananchi kukusanya maoni na mapendekezo yako dhidi ya namna gani katiba mpya iwe.

Zao la rasimu, ambalo linahitaji bado ushiriki imara na wa ukaribu wa kila raia katika kuisoma na kuielewa vyema nyaraka kwa kina na kutathmini mapendekezo hayo ya mjumuisho wa maoni ya wananchi na tafakuri ya tume katika maeneo mbalimbali.

Je hatua ya uhitaji wa kusoma kwa umakini na kuelewa rasimu ya katiba mpya utafanikiwa hasa tukitilia maanani viwango duni vya idadi ya wenye kujua kusoma na kuandika nchini Tanzania? Je tutamudu kupata maoni ya raia endapo wengi hawata soma na kusubiria kuhadithiwa?

Tukumbuke, Tanzania ina watu wasiojua kusoma takribani asilimia 24 kadiri ya takwimu za shirika la UNESCO 
mnamo mwaka 2010. Lakini pia, kwa wale ambao wanamudu kusoma na kuandika ambao ni asilimia 76 kadiri ya takwimu za shirika la UNESCO bado tunakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa tamaduni ya kujisomea na kuandika baina ya wanajamii wetu. Hivyo chapisho la rasimu ya katiba mpya lenye kurasa takribani 95 ikiwa na ibara jumla 240 inaweza kuwa shubiri kwa wengi kumudu kusoma kwa umakini.

Ni muhimu sana kufanya tafakari makini juu ya uhalisia wa raia wetu kwani ndipo tunaweza kubuni na kutekeleza njia madhubuti ambazo zitatuwezesha kufikia raia wengi zaidi wafahamu mapendekezo yaliyomo katika rasimu ya katiba.

Matukio mbalimbali ya hivi karibuni hasa katika utengenezaji wa sera na sheria yamedhihirisha hata kwa wale watendaji na wawakilishi wa wananchi ambao umakini wao unategemewa na wananchi wengi; wamekuwa wakishiriki kwa ufinyu kusoma kwa umakini na ndiyo maana tumekuwa tunasikia mara kwa mara wawakilishi waking'aka kuwa hawakuipitisha sheria kama hiyo au hawakuona kipengele hicho ambacho baada ya muda kimegundulika kikibana raia visivyostahili au kuikosesha mapato stahiki taifa.

Eneo la mikataba nalo ni sehemu nyingine ambayo ni taswira halisi ya taifa letu ambapo tumeshaona mikataba mingi yenye mashaka yaliyoibuliwa na kugundilika baada ya kusainiwa. Makosa yaliyo acha midogo wazi na kustaajabisha wananchi huku yakiibua maswali mengi hasa kuhoji kwanini mikataba ilitiwa sahihi na wataalamu na je kweli ilisomwa vyema kabla ya kusainiwa. Kiini cha yote ikidhirisha, kutokumudu kusoma kwa umakini na kufanya tafakuri ya kilichoandikwa.

Tayari tumeona baadhi ya juhudi ya kubaharisha ya kilichopo katika rasimu ya katiba mpya. Ni jitihada ambazo hazistahili kubezwa. Lakini pia, haziwezi kuachwa kujadiliwa na kutoa ushauri zaidi na zaidi mathalani upanuaji wa wigo wa mjadala wa kilichopendekezwa na rasimu ya katiba mpya zaidi ya mapendekezo yenye kugusa nyanja za kisiasa kama vile madaraka ya rais, aina ya serikali, masuala ya muungano.

Kuna masuala mengine mengi ambayo nayo yanahitaji sana jamii kuhabarishwa kwa kina hasa katika maeneo ya kijamii na kiuchumi. Namna gani Katiba Mpya itahakikisha inasimamia haki za kibinadamu na pia kutoa wajibu kwa kila raia wa Tanzania.

Tukumbuke mchakato mzima wa kuipitia rasimu ya katiba mpya upo ndani ya muda maalumu wenye ukomo ili kuenda sambamba na ratiba nzima ya mchakato wa katiba mpya. Ifikapo mwishoni mwa Agosti, 2013 ndiyo utakuwa mwisho wa kupokea maoni juu ya rasimu ya katiba mpya.

Kwa kupitia mabaraza ya katiba nchini yenye wawakilishi waliochaguliwa na wananchi sambamba na mabaraza ya katiba huru yaliyo chini ya taasisi mbalimbali kwa mujibu wa fursa iliyotolewa na tume ya katiba mpya; kuna wajibu mkubwa sana wa kuhakikisha wajumbe wa mabaraza na wananchi kwa ujumla wanasoma vyema kwa kina na kujadili ibara kwa ibara iliyomo katika rasimu na kufanya tathmini huku wakiongozwa na dira na mahitaji ya sasa na ya miaka zaidi ya hamsini ijayo kwa taifa letu.

Kuna jukumu kubwa sana kwa wale ambao wamebahatika kupata uwezo na elimu ya kusoma na kuandika, kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kiraia kusoma kwa umakini ili waelimishe wengine wengi ambao hawana uwezo wa kusoma na kuandika. Sambamba na uwezo wa kusoma, pia tunahitaji uwezo wa kiubunifu wa kuhakikisha kubuni vyema njia mbalimbali nje ya zile njia zilizokwisha zoeleka za makongamano na warsha kuwafikia kila raia kutoa ufahamu wa nini kilichomo katika rasimu ya katiba mpya na kupata mawazo yao.

Ni jukumu langu, ni jukumu lako!

Na Michael Dalali

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

Share this :

Related Posts

0 Comments