[wanabidii] Mapendekezo ya (CCM) kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya

Tuesday, July 23, 2013

Mapendekezo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wanachama na viongozi wake.

UTANGULIZI

1.1 Mnamo tarehe 03/06/2013 Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitangaza rasimu ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

1.2 Rasimu hii ya Katiba itajadiliwa katika mfumo wa aina mbili wa mabaraza:

Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, ambayo yameshaundwa na yatatoa maoni yake kupitia mikutano itakayoitishwa na Tume ya Marekebisho ya Katiba. Mabaraza haya yanasimamiwa na Tume yenyewe.

Mabaraza ya Asasi, Taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana kama vile vyama vya siasa na jumuiya za kidini na kadhalika. Mabaraza haya yanasimamiwa na Asasi au Taasisi husika.

1.3 Chama Cha Mapinduzi kimeshajiunda kama Baraza la Katiba la kitaasisi na kutambuliwa rasmi na Tume kwa barua Kumb.na. AB 76/386/57 ya tarehe 24/052013

1.4 Kwa kuzingatia kwamba Chama Cha Mapinduzi ni Taasisi muhimu na yenye masilahi makubwa katika upatikanaji wa Katiba Mpya, Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa iliyokutana mjini Dodoma Tarehe, 10/6/2013, pamoja na mambo mengine ilielekeza kwamba uandaliwe utaratibu utakaohusisha utoaji wa maoni utakaotumiwa na wanaCCM kutoa maoni yao.

1.5 Madhumuni ya ufafanuzi huu ni kujenga uelewa wa pamoja wa maudhui ya Rasimu ya Kwanza na hivyo kuwawezesha wanaCCM kushiriki kutoa maoni yao kikamilifu kutoka ngazi ya matawi hadi taifa.

UTARATIBU WA KUTOA MAONI

2.1 Kwa upande wa matawi maoni yatatolewa kupitia mikutano

Kwa wilaya, mikoa na taifa. Maoni yatatolewa kupita halmashauri kuu zao.

2.2 Ili kupata mfumo wa aina moja wa kuijadili Rasimu ya kwanza na kutoa maoni, wanachama wanaelekezwa kuzingatia vigezo vifuatavyo:

Kuitaja sura ya Rasimu ya Katiba inayohusika

Kutaja ibara ya Rasimu ya Katiba

Kutoa maelezo juu ya Ibara hiyo (kama kuna upungufu au maoni mengine yoyote);

Mapendekezo ya marekebisho

Sababu za mapendekezo ya marekebisho hayo.

MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA

3.1 Ieleweke kwamba hii ni rasimu ya kwanza ya Katiba na siyo Katiba rasmi au iliyokamilika. Baada ya maoni ya mabaraza ya Katiba ya Wilaya na kitaasisi itafuata rasimu ya pili itakayowasilishwa kwenye Bunge la Katiba. Mwisho kutakuwa na rasimu ya tatu itakayofikishwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni yao kwa uhuru na kwa kina.

3.2 Kwa mujibu wa mwongozo wa Tume, Wajumbe wa Mabaraza ya Wilaya wanaweza pia kushiriki kama Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya asasi au Taasisi ili mradi ni mwanachama wa Asasi au Taasisi husika. Kwa mantiki hii wanaCCM walioko kwenye mabaraza ya katiba ya wilaya wanahimizwa kushiriki kikamilifu kwenye ngazi husika za Mabaraza ya Katiba ya CCM kama taasisi.

3.3 Maoni yatakayotolewa kupitia mabaraza ya katiba yanatakiwa yawe yameifikia Tume ya Marekebisho ya Katiba kabla au ifikapo Agosti 31, 2013.

3.4 Katika awamu ya kwanza ya mchakato wa kutoa maoni Chama Cha Mapinduzi kiliandaa mwongozo wake uliojielekeza kwenye mambo makuu ya msingi na yenye masilahi ya pekee kwa Taifa letu.

3.5 Vivyohivyo katika kipindi hiki cha kutoa maoni juu ya Rasimu ya Kwanza, Chama Cha Mapinduzi kinawaelekeza wana-CCM kujadili kwa umakini maeneo hayo na kwa masilahi ya Taifa letu.

3.6 Ili kurahisisha utekelezaji wa wajibu huu, chama kinatoa muhtasari kwa maudhui yaliyomo katika sura zote 16 za Rasimu ya Kwanza ya Katiba na kugusa kwa kipekee Sura zinazohusu misingi mikuu ya Taifa letu.

MAUDHUI YA RASIMU YA KATIBA

4.1 UTANGULIZI

Utangulizi wa Rasimu ya Katiba unaeleza madhumuni ya kutungwa kwa Katiba Mpya, yakiwemo kuheshimu na kuendeleza Utu, Uhuru, Haki,Usawa, Udugu, Amani, Umoja, na Mshikamano.

Kadhalika Rasimu ya Katiba inasisitiza jukumu la kutunza mali na urithi wa nchi, utunzaji wa mazingira endelevu na rasilimali za Taifa, kupiga vita uharibifu na ubadhirifu kuendeleza amani na kutambua nafasi ya Tanzania Kikanda na barani Afrika.

Kupitia Rasimu ya Katiba hii wananchi wa Tanzania wajizatiti kuendeleza Muungano, kujenga Taifa huru lenye kutambua Utawala wa Sheria , Maadili, Uwajibikaji na Uwazi, Umoja Mshikamano, kuendeleza umuhimu wa mamlaka ya watu na ukuu wa Katiba.

WanaCCM wako huru kutoa maoni yao juu ya sehemu hii ya utangulizi

SURA YA KWANZA (Ibara ya 1-9)

Sura hii inatambulisha kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na imegawanywa katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inaeleza kuhusu mipaka, alama lugha, utamaduni, na Tunu za Taifa.

Sehemu ya pili ya sura hii inaelekeza kuhusu Mamlaka ya Wananchi, utii na hifadhi ya Katiba. Kwa mujibu wa Rasimu, wananchi ndio msingi wa mamlaka ya nchi na Serikali inawajibika kwa wananchi.

MAONI:

Ibara ya 1(1) inazungumzia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maneno yaliyotumika "Shirikisho lenye mamlaka kamili" inapendekeza yatolewe na badala yake yasomeke "Jamhuri ya Tanzania ni nchi yenye mamlaka kamili ambayo imetokana na …."

SABABU: Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuelezeka kuwa ni shirikisho bali ni nchi yenye mamlaka kamili.

(ii) Ibara ya 1 (2) inataja Jamhuri ya Muungano kuwa ni shirikisho. Maneno yaliyotumika'Jamuhuri ya Muungano ni shirikisho la …..' inasomeka yasomeke Jamhuri ya muungano ni nchi ya ……'

SABABU: Kama zilivyoelekezwa hapo juu kwenye(1)

Ibara ya 3(2) inazungumzia Siku Kuu za Taifa. Inapendekezwa sikukuu za Taifa zitajwe kwenye sheria badala ya Katiba.

SABABU: Siku kuu za kitaifa zinaweza kubadilika kwa kuongezeka au kupungua itakuwa rahisi kuifanyia sheria marekebisho kuliko Katiba ambayo utaratibu wa kuifanyia marekebisho huchukua muda mrefu.

(iv) Ibara ya 5 (e) imetaja uwazi kama mojawapo ya Tunu za Taifa. Neno Uwazi inapendekezwa liondolewe na badala yake yawekwe maneno 'Usawa wa Binadamu'

SABABU: Uwazi si moja wapo ya Tunu za Taifa?

Ibara ya 8 (1) inazungumzia mamlaka ya utii wa Katiba. Maneno ' Bila ya kuathiri masharti ya Katiba za Washirika wa Muungano kwa mambo yasiyo ya Muungano inapendekezwa yaondolewe na isomeke kama ' Katiba hii itakuwa sheria kuu katika Jamhuri ya muungano'

SABABU: Katika muundo wowote wa Muungano, Katiba ya Muungano ndiyo Sheria Kuu.

4.3 SURA YA PILI (Ibara ya 10-12)

Sura ya pili inaeleza malengo muhimu, misingi ya mwelekeo wa shughuli za Serikali na sera za kitaifa. Sura hii inaweka mwongozo kwa serikali na sera za kitaifa. Sura hii inaweka Mwongozo kwa Serikali, Bunge, Mahakama, Vyama vya Siasa na Taasisi na Asasi.

MAONI:

Ibara ya 11(2) na (3) vinavyohusu utekelezaji wa malengo ya Taifa viondolewe.

SABABU: Malengo ya kitaifa yaliyotajwa katika ibara 11 (3)(a) kisiasa (b)kijamii (c) kiuchumi (d)kiutamaduni (e) kimazingira yanapaswa kuainishwa kwenye sheria mbalimbali za nchi washirka wa Muungano.

Sura hii inatoa dira na mwelekeo wa shughuli za serikali. WanaCCM wajadili na kutoa maoni yao.

Inaendelea uk.36

4.4 SURA YA TATU Ibara ya (13-21)

Sura ya tatu ina sehemu mbili zinazoweka Maadili na Miiko ya Uongozi wa Umma. Sura hii imeweka vigezo kwa watu wenye dhamana kujilinda wakiwa katika shughuli za kazi au za binafsi, kuepusha mgongano wa masilahi binafsi na ya Ofisi; na kuepuka vitendo vinavyoweza kushusha hadhi ya ofisi za umma. Mambo ya msingi yanayotajwa katika sura hii ni pamoja na suala la Rushwa, kujilimbikizia mali na utunzaji wa siri za Serikali.

MAONI:

SURA YA TATU YOTE, inayohusu Maadili ya Viongozi wa Umma iwekwe katika Sheria inayotungwa maalumu kwa ajili ya kuainisha maadili na miiko ya viongozi wa umma.

SABABU: Maadili miiko na utumishi wa umma inaweza kuimarishwa kwa kufafanuliwa au kuongezwa vipengele vipya kwa urahisi zaidi kuliko ikikaa kwenye Katiba ambayo utaratibu wake wa marekebisho ni mrefu.

Sura hii inaweka misingi ya kusimamia uadilifu katika utumishi wa umma, WanaCCM wajadili na kutoa maoni yao.

4.5 SURA YA NNE (Ibara ya 22-53)

Sura hii ina sehemu kuu mbili zinazozungumzia Haki za Binaadamu, Wajibu wa Raia na Mamlaka za Nchi.

Ibara ya 31 inayohusu uhuru wa imani ya dini iimarishwe kwa kuandikwa upya. Itamke bayana kuwa Serikali ya Jamhuuri ya Muungano haina dini. Ndani ya Katiba itajwe misingi mikuu ya imani ya dini kama vile ibara ndogo za (1)-(5). Ibara ndogo ya (3) iimarishwe kwa kuongezwa ufafanuzi au vipengele vitakavyohusu mwenendo wa viongozi na ushiriki wao rasmi katika shughuli za dini kwa namna ambayo itatenganisha nyadhifa za kiserikali katika shughuli hizo na ushiriki wao kama mtu binafsi.

SABABU: Mwenendo ulivyo hivi sasa ni viongozi kushiriki katika shughuli za kidini kwa nyadhifa zao kiasi kwamba si rahisi kutenganisha sura ya Serikali na sura ya dini ya mtu binafsi.

Ibara ya 42 inayozungumzia haki ya mtoto iboreshwe ili itambue kimsingi haki za msingi za mtoto. Lakini ziainishwe kwa ufasaha katika Sheria ya Mtoto.

SABABU: Haki za mtoto ni nyingi kuliko hizo zilizotajwa kwenye Rasimu ya Katiba, na isingewezekana kuzitaja zote. Ili hili lifanikiwe itakuwa rahisi zikiwemo kwenye Sheria ambayo itaziainisha zote na kuzifafanua vizuri zaidi.

Ibara ya 46 (1)(d) inayohusu haki za wanawake iboreshwe ili isomeke 'kupata ujira sawa kwa kazi inayofanana'

SABABU: Kutoa ufafanuzi kwamba dhana ya ujira sawa kati ya mwanamke na mwanamume inahusu watu wenye sifa sawa na kazi inayolingana.

Ibara ya 50-53 zina vipengele vingi vinavyohusu haki za binadamu. Inapendekezwa kuwa ibara hizi zifupishwe na zirudishwe katika sura ya nne ya Rasimu hii inayohusu Haki za Binadamu ya Sehemu ya Kwanza.

SABABU : Uandishi mzuri wa sheria ni kuhakikisha vipengele vya aina moja vinapatikana sehemu moja, kwa urahisi na kwa lugha nyepesi.

Haki hizi zimefafanuliwa na kuimarishwa kwa kuingiza haki za watoto, vijana, wazee na wanawake. WanaCCM wajadili na kutoa maoni ya o.

4.6 SURA YA TANO (Ibara ya 54-56)

Sura ya Tano inazungumzia uraia wa Jamhuri ya Muungano . Sura hii ina maeneo mapya yanayofafanua nani anaweza kuwa Raia wa Tanzania. Inalinda watoto ambao watakuwa nchini wakiwa chini ya umri wa miaka saba bila ya wazazi wao kujulikana, na watoto walioasiliwa na raia wa Tanzania. Pia Rasimu inaweka masharti ya kuomba kwa mtu aliyefunga ndoa na raia wa Tanzania kuweza kuomba uraia.

Rasimu inaendeleza uraia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyo Katiba ya sasa.

MAONI

Sura ya Tano inayohusu uraia katika Jamhuri ya Muungano wa liongezwe suala la uraia wa nchi mbili.

SABABU: Kuwawezesha Watanzania waishio ughaibuni kunufaika na fursa zinazopatikana katika nchi walizomo ikiwa wataamuia kuwa raia wanamofanyia kazi.

WanaCCM wajadili kutoa maoni yao .

4.7 SURA YA SITA (Ibara ya 57-66)

Sura hii inapendekeza Muundo wa Mpya wa Jamhuri ya Muungano, Sura inaeleza kuwepo kwa Jamhuri ambayo mfumo wake utakuwa ni wa Shirikisho linaloundwa na Serikalio tatu (Ibara ya 57) (1) :Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanzania Bara.

Aidha sura hii inaeleza kuwa kuwa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muuungano zitatekelezwa na kusimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano; Bunge la Jamhuri ya Muungano; na Mahakama ya Jamhuri ya Muungano .

Pendekezo hili ni tofauti na Sera ya Chama Cha Mapinduzi ya Muundo wa Muungano wenye Serikali mbili ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Muundo huu wa Serikali mbli ulitokana na makubaliano ya nchi mbili huru ambazo zilikuwa ni Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ya mwaka 1964.

MAONI

Ibara ya 57 inahusu Muundo wa Muungano wa Shirikisho lenye Serikali tatu inapendekeza Jamhuri ya Muungano iwe nchi yenye muundo wa Serikali mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa maana hiyo, ibara ya 57(1) (c) na ibara ya 53(3) ziondolewe ili shughuli za kiutendaji zinazohusu Tanzania Bara. Zisimamiwe na Serikali ya Jamhuri na zile za Zanzibar zisimamiwe na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

SABABU

I. KISHERIA

(i)Msingi mkuu wa Muungano kati ya iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri yua Watu wa Zanzibar ni wa Serikali mbili kwa mujibu wa Makubaliano ya 1964, Mapendekezo ya Rasimu yanafanya rejea kwenye Makubaliano 1964 ambayo msingi wake si Serikali tatu.

(ii) Mfumo wa Serikali tatu utaleta urasimu na utata wa kisheria katika umiliki na uendeshaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii;

(iii) Kusababisha mgogoro wa kisheria kuhusu masuala ya uwakilishi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano kwani majimbo ya uchaguzi yatakuwa mikoa kwa Bara na mikoa kwa Zanzibar wakati uundwaji wa mikoa na wilaya si jambo la Muungano.

II. KISIASA

(i)Serikali ya Jamhuri ya Muungano itaelea kimadaraka na kimamlaka kwa sababu haitakuwa na uwezo wa kushughulikia moja kwa moja masuala ya yanayohusu wananchi- kwa mfano elimu, afya, kilimo, maji barabara, kwani siyo ya Muungano ingawaje katika Rasimu hii ya Katiba yanazungumzwa kama sehemu ya majukumu ya Serikali ya Muungano;

(ii)Kutokana ukubwa wa eneo na uchumi wa Tanzania Bara ni wazi kwamba itachangia zaidi kwenye uendeshaji wa Serikali ya Muungano hii inaweza ikatoa mwanya kwa Serikali ya Tanzania Bara kuiburuza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Jambio hili litadhoofisha Muungano na uhuru wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

Share this :

Related Posts

0 Comments