[wanabidii] CHADEMA: HATUTASHIRIKI KONGAMANO LA AMANI

Monday, July 08, 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu waandishi wa habari,
Tumewaiteni hapa mchana huu kwa dharura, kutokana na kujitokeza kwa jambo moja muhimu sana katika mustakabali wa chama chetu na taifa kwa ujumla. Jambo lenyewe ni hili:
Kwa muda wa siku mbili, kuanzia kesho– tarehe 9 Julai 2013 hadi 10 Julai – kutakuwa na "KONGAMANO LA AMANI" lililoitishwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania – Tanzania Center For Democracy (TCD).
Kongamano hilo litajadili na kutafakari Amani ya Taifa, litafanyika kwenye hoteli ya White Sands ya jijini Dar es Salaam. Litafuguliwa na Mwenyekiti wa TCD, Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Mheshimiwa James Mbatia na litafungwa na Rais Jakaya Kikwete.
Baadhi ya washiriki, ni pamoja na mawaziri, viongozi wakuu wa vyama vyenye wabunge ambavyo ni wanachama wa TCD – Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Wananchi (CUF), United Democracy Party (UDP), Tanzania Lebour Party (TLP), NCCR- Mageuzi na CHADEMA. 
Aidha, chama cha UPDP nacho kitashiriki mkutano huo kwa niaba ya vyama vingine ambavyo havina wabunge.
Ndugu waandishi wa habari,
CHADEMA kikiwa mmoja wa wadau wakubwa wa TCD, kimepokea mwaliko wa mkutano huo. Hata hivyo, tunapenda kutumia nafasi hii, kupitia kwenu, kuutangazia umma na Watanzania wote wanaotutakia mema na kulitakia mema taifa hili, kwamba hatutashiriki mkutano huo kwa sababu zifuatazo:

Kwanza, Mwenyekiti wa TCD, Mheshimiwa Mbatia kwa makusudi amekiuka maazimio ya kikao ya kuteuwa Mwezeshaji wa mkutano huo na badala yake akafungamana na CCM kuteuwa watu wanaowataka wao.
Pili, Chadema haitashiriki mkutano huo kwa kuwa Amani haijadiliwi. Amani inatengenezwa na kuwapo kwa mazingira ya haki na usawa; na kwamba aliyebobea katika uvunjaji wa haki hizo, ni serikali yenyewe. 
Katika mazingira haya, CHADEMA inaona hakuna umuhimu wa kushiriki kwenye mkutano ambao washiriki ni wale wale wanaotuhumiwa kuvunja haki za binadamu.
Tatu, Amani siyo ya vyama vya siasa pekee yake. Amani inahusisha wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa kidini, taasisi za kiraia na mashirika yasiokuwa ya kiserikali. Taarifa zilizopo, ni kwamba mkutano huu haukushirikisha viongozi wa kidini, na hivyo, tunadhani kuwa siyo jambo zuri kama kweli tunataka kutafuta amani ya taifa.

Nne, Chadema haitashiriki mkutano huo kwa kuwa aliyepanga, aliyefadhili na aliyeitisha mkutano huo kwa mgongo wa TCD, ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Mizengo Kayanza Peter Pinda, ambaye ndani ya nafsi yake, haonekani kuwa na dhamira ya dhati ya kuwapo amani katika taifa letu.
Ndugu waandishi wa habari;
Ninyi ni mashahidi wa jinsi Waziri Mkuu Pinda alivyo mstari wa mbele katika kuhubiri kauli za chuki, uhasama, uchochezi, ubabe na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini. Siyo mara moja wala mbili, Waziri Mkuu Pinda amesikika, tena ndani ya Bunge, akihamasiha vyombo vya usalama kuvunja sheria kwa kupiga, kuteka na kung'oa meno watu wanaotumia haki zao za kikatiba kushinikiza serikali kuchukua hatua dhidi ya maovu.

Tano, CHADEMA haitashiriki katika mkutano huo kwa kuwa Serikali ya CCM inayofadhili mkutano huu, imejaa unafiki kwa kuhubiri amani mchana, wakati usiku inachochea uhasama wa kidini, kisiasa na inawagawa Watanzania kwa misingi ya imani za kidini na vyama.
CHADEMA inao ushahidi usio na chembe ya mashaka, kwamba mifarakano mingi inayotokea kwenye jamii, mapigano katika koo mbalimbali, ugomvi wa kugombea ardhi kati ya wakulima na wafugaji, machafuko kwenye mikutano ya hadhara ya vyama vya upinzani, sababisho lake kuu ni CCM kuvitumia vyombo vya dola, ili kukibeba chama hicho.

Tunataka umma utuelewe, kwamba tuna dhamira ya dhati ya kuona Tanzania inakuwa kisiwa cha amani, lakini hatutakubali kushiriki katika vikao ambavyo wanaoviongoza hawana dhamira hiyo. Ili amani iweze kupatikana, ni sharti kuwepo mijadala inayoingia kwenye viini vinavyosababisha amani ikosekane na hatua hiyo ianze kuchukuliwa na ionekane inachukuliwa na serikali.

CHADEMA iko tayari, kufanya kazi ya kutafuta amani na wale wanaopenda demokrasia. Chadema haifanyakazi na wanafiki wa amani.

Imetolewa na:
Benson Singo Kigaila,
Mkurugenzi wa Oganaizesheni ma Mafunzo, 
Dar es Salaam

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments