[Mabadiliko] Ewe Obama, tatizo letu kubwa Afrika ni ubaguzi wa kisiasa ( Makala, Raia Mwema)

Friday, July 05, 2013


Na Maggid Mjengwa,

" WAAFRIKA waijenge Afrika yao, kwa ajili ya Afrika!" Anasema Barack Obama. Ni dhana njema, lakini, unafanyaje pale Waafrika wenyewe wanagombania fito katika kuijenga Afrika yao?

Naam, Afrika wajenzi walio juu kwenye paa wanapokea fito kwa kuangalia imeletwa na nani. Inahusu ubaguzi wa kisiasa. Na hapa ndipo ilipo changamoto kubwa ya maendeleo ya bara hili.

Na kwa nchi yetu, ili tupige hatua za maana za maendeleo, Watanzania na hususan viongozi, waifanye sasa  kazi ya kuondokana na ubaguzi wa kisiasa katika nchi yetu.  Ubaguzi huu wa mathalan, ' Hawa ni wenzetu' na ' Wale ni maadui zetu' umejengeka katika misingi ya kulindana katika maovu.  Wenye kuendekeza ubaguzi huu  ndio wenye kudhihirisha kile Rais Kikwete mwenyewe alipata kukitamka mwaka 2005- kugombania fito wakati tunajenga nyumba moja.  

Nimepata kuandika, kuwa kiongozi anapaswa kuwa na maono ama visheni ya anakotaka kuipeleka nchi. Na  kiongozi wa nchi ataangalia sana juu ya uchumi wa nchi. Kinachofuatia ni kwa kiongozi kuitumia siasa kama nyenzo katika kutimiza maono na malengo ya kiuchumi kwa nchi.


Na Jeffrey Sachs ni Mwanauchumi maarufu ambaye Jakaya Kikwete amepata kukutana na kuongea naye kwenye Ikulu yake. Profesa Jeffrey Sachs ana mfano hai wa Poland.  Katika kuwashauri  kuinuka kiuchumi WaPoland wale , Profesa Sachs aliwaambia; " Political power must be shared".  Kwamba kuna umuhimu wa vyama kuwa na utayari wa kugawana madaraka ya uongozi wa kisiasa.

 
Ndio, Fundi Umeme yule Lech Walensa wa chama cha wafanyakazi na aliyeanzisha vuguvugu la mapinduzi ya kujikomboa kutoka Ukomunisti nchini Poland aliambiwa na Profesa Jeffrey Sachs; "  Chama chako cha Solidarity kiwe radhi kuunda Serikali ya Mseto na Chama Cha Kikomunisti". Na ikawa hivyo, kimoja kikatoa Waziri Mkuu na kingine Rais.  Kukawepo utulivu wa kisiasa. Poland ikaanza kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi. Ndio, hakuna uchumi unaokua bila uwepo wa utulivu wa kisiasa.


Maana tunakumbuka siku ile Rais Kikwete  alipotangaza mpango wa kiuchumi wa miaka mitano kule Dodoma, Kikwete alitamka;  " Bila Utawala Bora , bila kuwa na demokrasia, bila kuheshimu Haki za Kibinadamu,  mafanikio ya kiuchumi hayatawezekana."

 
Rais  hakupigiwa makofi  ya nguvu. Ndio, wengi wa viongozi waliokuwa wakimsikiliza Rais kwenye ukumbi ule wa Saint Gasper pale Dodoma ni Wana-CCM. Bila shaka kuna waliokuwa wakifikiria Ukuu wa Wilaya wao na Ukuu wao wa Mkoa. Walifikiria nyadhifa  zao. Mambo ya kupanua demokrasia ikiwamo uwepo wa  vyama vingi  kwao ina tafsiri ya kutishia vibarua vyao!

Na changamoto ya kauli ya Obama kwa Waafrika inaanzia kwa historia ya marehemu baba yake, Barack Hussein Obama, Sir. Huyu alikuwa mmoja wa wahanga wa ubaguzi wa kisiasa katika Kenya ya Mzee Kenyatta.


Naam,
Obama anaipenda Afrika, ni bara alilozaliwa baba yake mzazi, Dr. Barack Hussein  Obama, Sir. Hivyo, kwa Barack Obama, Afrika ni bara la asili yake, na Kenya ndiko iliko asili yake. Ndiko liliko kaburi la baba yake.

Lakini, Obama ana simulizi  mbaya juu ya bara hili na hususan inapohusu demokrasia na uhuru wa watu kujieleza. Obama hahitaji kutoa mifano ya wengine anapozungumzia wahanga wa kukosekana kwa demokrasia. Obama ana mfano wa baba yake mwenyewe wa kumzaa; Dr. Barack Hussein Obama.

 

Baba yake alikufa kwenye ajali ya gari Nairobi, lakini, ni matokeo ya kuandamwa na mfumo kwenye Serikali ya Mzee Jommo Kenyatta, kwa vile tu, baba yake Obama alikuwa anafikiri tofauti na watawala. Na mwishowe alikuwa anatembea na siri ya aliyemwua mwanasiasa Tom Mboya.  Aliitwa na mamlaka na akaambiwa; " Funga Mdomo!"

 

Baba yake Obama alikuwa rafiki wa karibu sana wa Tom Mboya aliyeuawa katika mazingira ya kutatanisha. Lakini, inaaminika, aliuawa kwa vile alifikiri tofauti na watawala.  Kwenye kitabu kiitwacho; ' The Bridge' kilichoandikwa na mwandishi David Remnick, mwandishi anaelezea siku ambayo Jommo Kenyatta alifika Kisumu na kupokewa na kelele za wananchi wakimwuliza;

" Tom yuko wapi?" " Tom yuko wapi?"

 

Jambo hilo lilimwaibisha sana Jomo Kenyatta. Akalaumu chama cha Jaramong Odinga cha KPU- Kenya People's Union kwa kuwagawa wananchi. Naye Rais Kenyatta akatamka hadharani; " Odinga ni rafiki yangu, lakini anawapotosha wananchi, na anaendelea kuwapotosha watu wa eneo hili. Tutawapondaponda muwe kama unga. Yeyote anayecheza na maendeleo yetu tutamwangamiza kama nzige. Msije mkasema sijawaonya."

 

Baada ya hapo gari la Kenyatta lililondoka mahali hapo kwa kasi  huku umati ukilirushia mawe. Polisi hawakurusha mabomu, bali, walilengesha mitutu yao ya bunduki kwenye umati ule .  Watu tisa tisa walikufa hapo hapo na wengine sabini kujeruhiwa.

Siku mbili baadae  Kenyatta akawamata Jaramongi Odinga na viongozi wengine kadhaa wa KPU. Walishtakiwa  kutaka kumpindua Rais Jomo Kenyatta. Odinga akawekwa jela kwa miaka miwili, na kila msomi mwenye asili ya Kijaluo alionja joto ya jiwe. ( The Bridge, David Remnick, page 67-68)

 

Hayo machache tu kwenye simulizi mbaya ya Obama juu ya Afrika, yanamfanya Barack Obama kuwa wakili mtetezi wa kweli wa kupigania demokrasia katika Afrika.  Hivyo, Obama anaposisitiza umuhimu wa uwepo wa demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari barani Afrika anamaanisha anachosema na hasemi asichomaanisha.

 

Na hapa tuyakumbuke maneno ya Obama pale alipotoa hotuba ya kutawazwa kuwa Rais wa Marekani kwa mara ya pili. Obama alisema;

 

" Taifa la Marekani ni mahali ambapo kila mmoja ana nafasi ya kutimiza ndoto yake. Ndoto ya kuwa yeyote yule, bila kujali rangi, dini au jinsia yako. Wakati tukiyaongea haya hapa, kuna wanadamu wenzetu mahali pengine duniani  wako gerezani kwa kosa la kufikiri tofauti. Kwa kosa la kuonyesha dhamira ya kutimiza ndoto zao."- Barack Obama.

 

Naam, kuna mahali fulani hata Barack Obama anajua, kuwa kama angeliishi Kenya, kwenye nchi ya baba yake, na kuwa na ndoto ya kuwa Rais wa Kenya. Akaitamka hadharani na kuonyesha kwa matendo, basi, huenda, sio tu angefungwa gerezani kwa kufikiri tofauti na watawala, bali, huenda leo  angeshakuwa amezikwa kando ya kaburi la baba yake kule Kogelo, Kisumu, Kenya.

 

 Obama  aendelee kuwa wakili wa kweli wa kutetea demokrasia kwenye bara la asili ya baba yake. Ni pamoja na kufuta ubaguzi wa kisiasa. Ni kwa vile, bila uwepo wa demokrasia ikiwamo uhuru wa kujieleza, Afrika itabaki kuwa bara la giza. Tuna nafasi na kila sababu za kurudisha nuru kwenye bara hili. 

 Mungu Ibariki Afrika.

http://mjengwablog.com

--
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda; mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com
Utapokea Email ya kudhibitisha kujiondoa kwako.
 
TEMBELEA Facebook yetu:
http://www.facebook.com/MabadilikoForums?ref=hl
 
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
 
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forums" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

Share this :

Related Posts

0 Comments