[wanabidii] WALIOFAULU NI 6.4% TU

Thursday, February 21, 2013
Matokeo ya kidato cha nne yameleta simanzi kubwa kwa watanzania wengi, hasa ndugu, jamaa na marafiki wa watoto waliojiua, wazazi na wanafunzi waliokuwa na mategemeo makubwa ya kuona mwanga wa maisha yao kwa kupitia mlango wa elimu. Vyombo vya habari vimeripoti kuwa wanafunzi watatu wamejiua kutokana na kupata matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu.
 
Ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kidato cha nne kwa mwaka huu ni kama ifuatavyo;
 
DIVISION ONE:     1,641
DIVISION TWO:     6,453
DIVISION THREE: 15,421
DIVISION FOUR:     103,327
DIVISION ZERO:     240,903
 
Kwa matokea haya, wanafunzi waliopata Daraja la 1-3 ni 23,515 tu kati ya jumla ya wanafunzi 367,745 waliofanya mtihani. Kwangu mimi, siwezi kuhesabu wanafunzi waliopata daraja la 4 kuwa wamefaulu. Katika daraja la 4, kuna wanafunzi wengi ambao wana alama ambazo haziwaruhusu kujiunga na chuo chochote ambacho huchukua wanafunzi waliofaulu mtihani wa kidato cha 4. Utasemaje kuwa wanafunzi hao kuwa wamefaulu? Kwa hiyo, kwa uhakika tunaweza kusema kuwa wanafunzi waliofaulu ni 6.4% pekee.
 
Swali la kujiuliza, hivi inawezekana kweli kati ya wanafunzi 367,745 ni wanafunzi 23,515 tu ndiyo wenye uwezo wa kuelewa wakifundishwa? Ukweli ni kwamba, watanzania wote wanaamini kuwa kuna wanafunzi wengi kati ya hao 344,230 waliofeli walikuwa na uwezo wa kufaulu, walikuwa na haki ya kufaulu lakini hawakufaulu, siyo kwa sababu hawana akili bali ni kwa sababu walitengenezwa mazingira ya kutokufaulu.
 
Watu wengi wameongelea juu ya Rais kumfukuza kazi Dr. Shukuru Kawambwa au yeye mwenyewe kujiuzulu, mimi naunga mkono hoja hiyo. Kufanya hivyo kutaonesha kuwa Rais amekasirishwa na matokeo haya, na anaungana na Watanzania waliochukizwa na matokeo haya kuomboleza msiba huu wa kielimu. Lakini pia Rais atakuwa anapeleka ujumbe mzito kwa Mawaziri wengine kwamba kila atakayepewa wizara hiyo kuwa haendi kupumzika bali kwenda kufanya kazi ya kubadilisha mwenendo wa maendeleo ya sekta nzima. Tunajua kuwa kufukuzwa kwa Dr. Shukuru Kawambwa hakutabadilisha matokeo ya wanafunzi waliofeli lakini utakuwa ujumbe tosha kwa Watanzania kuwa hata Rais hakufurahishwa na matokea haya.
 
Sekta ya Elimu, ni sekta Mama ambapo kila mmoja alitegemea kuwa sekta hiyo daima ingeongozwa na mtu mwenye uwezo wa hali ya juu na mwenye historia ya ufanisi ya utendaji kazi. Watanzania tulio wengi tulishangazwa sana Mh. Rais alipompa wizara hiyo Dr. Shukuru Kawambwa.
 
Wakati tunaomba Rais kumfukuza kazi Dr. Shukuru Kawambwa ni muhimu sana kuongelea hatima ya hili kundi kubwa la wanafunzi waliofelishwa, kufanyike nini ili kuwaokoa, maana hawa ni Watanzania, ni watoto wa Watanzania, ambao walikuwa na haki na bado wana haki ya kuyafurahia maisha yao ya sasa na baadaye, wana haki ya kuyafikia malengo yao ya kimaisha LAKINI kutokana na makosa mbalimbali ya serikali na jamii yetu wapo hapo walipo. Ni lazima tuongelee namna ya kuwaokoa. Watoto hawa watakuwa mzigo kwa wazazi wao, kwao wenyewe na familia zao huku mbeleni, kwa Taifa na jamii yetu wote. Ni lazima tujadlili sasa namna ya kupunguza athali ya mzigo huu.
 
Napendekeza serikali ifanye program maalum ambapo watoto hawa waliofelishwa warudi mashuleni wafundishwe kwa muda wa miezi 6 na kisha wafanye mtihani mwingine, kwa sababu nina uhakika kuna wengi wenye uwezo wa kufaulu katika hilo kundi kubwa. Wizara na serikali waangalie hilo linaweza kufanyika kwa namna gani.
 
Dr. Shukuru Kawambwa ni lazima afukuzwe kama njia ya kupeleka ujumbe kwa Mawaziri wote na watendaji wengine kuwa unapopewa dhamana kuna wajibu unaoambatana nao na pia kuna matarajio ya Watanzania. Ukishindwa kuyafikia, ni lazima uwajibishwe. Rais tutamshangaa sana kama hatamfukuza Dr. Shukuru Kawambwa. Ikumbukwe kuna wanafunzi waliojiua kutokana na matokeo haya. Na mara nyingi wanafunzi wanaofadhaishwa na matokeo mabaya ni wale ambao walikuwa na mategemeo makubwa ya kufanya vizuri, na huchanganyikiwa baada ya matokeo kuja kinyume chake. Wanafunzi hawa wanaoweza kuchukua uamuzi kama huo, ni wale ambao, mara nyingi waliojitahidi kufanya maandalizi kwa kiwango chao cha juu kabisa, ambao huwa wanatoka familia duni, wakitegemea kuwa elimu inaweza kubadilisha maisha duni ya familia zao, kisha wanaona kuwa ndoto zao zimezimika ghafla.
 
Kama Mheshimiwa Rais hawezi kumfukuza Dr. Shukur Kawambwa kwa kuwafanya wanafunzi karibu wote kufeli mwaka huu, basi amfukuze kwa wizara yake kusababisha wanafunzi kupoteza maisha kwa kujiua kwa kujiua kutokana na matokea manaya ya mitihani yao.
 
Bart

Share this :

Related Posts

0 Comments