WIKI iliyopita, tulianza kuwaletea historia ya mwanasiasa machachari na kiongozi pekee wa serikali aliyejitoa mhanga kuwakabili wanajeshi walioasi mwaka 1964.
Wiki hii tunaendelea na makala hii, ambayo itaonyesha pamoja na kuwa waziri katika serikali ya Mwalimu J. K Nyerere na kufanya mambo mengi makubwa, kwa nini sasa amesahaulika? Endelea.
Wiki hii tunaendelea na makala hii, ambayo itaonyesha pamoja na kuwa waziri katika serikali ya Mwalimu J. K Nyerere na kufanya mambo mengi makubwa, kwa nini sasa amesahaulika? Endelea.
L-R: Kambona, Kawawa, Kenyata, Nyerere (picha: juliusnyerere.info)
Ugomvi wa Nyerere, Kambona
Vyanzo mbalimbali vya habari hadi sasa vinashindwa kueleza ukweli juu ya hasa kile kilichosababisha kuzuka kwa tofauti kati ya Mwalimu Nyerere na Kambona.
Kila mtu amekuwa akijaribu kueleza ugomvi wa wawili hawa kadiri ajuavyo.
Kuna madai kwamba viongozi hawa wawili ambao kwa sasa wote ni marehemu, walianza kutofautiana baada ya maasi ya wanajeshi.
Inadaiwa kuwa Nyerere alitaka kuanzisha mfumo wa chama kimoja nchini ili kuimarisha usalama na Kambona alipinga hoja hiyo kwa maelezo kwamba mfumo huo ungezorotesha uhuru na maendeleo ya demokrasia. Hoja hiyo ikafikishwa bungeni kwa maamuzi na kwa bahati mbaya kwa Kambona akashindwa lakini akagoma kusaini muswada huo.
Katika safari ya China ya Mwalimu ya mwaka 1965, alipendezwa na mfumo wa kikomonisti wa Mao, na akataka kuanzisha mfumo kama huo kwa jina la 'Ujamaa' hapa nchini.
Dhana ya msingi ya mfumo wa Ujamaa ilikuwa ni kuwahamishia watu katika vijiji vya ujamaa na kutaifisha viwanda na vitegauchumi vilivyokuwa vikimilikiwa na watu binafsi ili kuwa chini ya wananchi, hatua iliyopingwa vikali na Kambona kwa maelezo kwamba ungeongeza umaskini na udhibiti wa serikali kwa watu.
Inadaiwa kuwa kulikuwa na msuguano mkali, kiasi kwamba ilimlazimu Kambona alijiuzulu nyadhifa zake ndani ya serikali na chama na hatimaye yeye na familia yake wakakimbilia Nairobi, Kenya na kisha Uingereza ambako walipatiwa hifadhi ya kisiasa.
Mara baada ya kukimbia nchi, mali za Kambona zilichukuliwa na serikali, huku ndugu zake wawili, wakiwekwa kizuizini bila ya kufikishwa mahakamani na kufungwa kwa zaidi ya miaka kumi.
Inaaminika kuwa wazo la Kambona lilikubaliwa na baadhi ya viongozi wa chama na serikali.
Hii inatokana na kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake, Bibi Titi Mohammed, Michael Kamaliza ambaye alikuwa mwanaharakati wa chama cha wafanyakazi, mwanachama wa TANU na waziri, pamoja na Gray Mattaka, Eliya Chipaka na Prisca Chiombola kwa tuhuma za uhaini.
Viongozi hao walihukumiwa pamoja na Kambona licha ya kuwa alikimbilia London lakini walikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Afrika Mashariki na wakaachiwa huru.
Hata pamoja na kuachiwa huru,walikamatwa na serikali na kufungwa tena.
Tuhuma kubwa ya Kambona ni kwamba aliiba pesa nyingi za umma, na kukamatwa nazo alipopekuliwa katika uwanja wa Embakasi, mjini Nairobi jambo ambalo alilipinga kwa miaka mingi na kuliweka wazi katika taarifa yake kwa waandishi wa habari Septemba 6, 1967 huko London. Kambona alikwenda mbali zaidi akaitaka serikali ya Tanzania kuiomba Kenya kutoa ukweli juu ya jambo hilo, jambo ambalo halikufanyika hadi kifo chake.
Inaaminika kuwa maisha ya Kambona jijini London yalikuwa ya shida na dhiki. Mwaka 1982, baadhi ya ndugu wa Kambona waliachiwa toka kizuizini baada ya juhudi za Waziri Mkuu wa New Zealand, Robert Muldoon.
Mwaka 1990, Kambona akiwa na matumaini makubwa ya mabadiliko ya kisiasa katika Tanzania, aliunda chama kiitwacho Tanzania Democratic Alliance, akiwa bado uhamishoni.
Kurudi Tanzania
Mwaka 1992, wakati mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa Tanzania, Kambona aliomba kurudi nchini.
Hata hivyo, serikali ya Tanzania ilimkatalia katakata. Kuona hivyo, Kambona aliiomba serikali ya Uingereza kumpa pasi ya kusafiria kurudi Tanzania, lakini pia akakumbana na tishio la kukamatwa na kuwekwa ndani pindi angelitua.
Septemba 5, 1992, bila woga wa kukamatwa, Kambona alitua katika ardhi ya Tanzania na hakushikwa, badala yake alipewa miezi mitatu awe amekamilisha utata wa uraia wake.
Nia yake ya kushiriki kwa nguvu katika harakati za siasa ilitiwa doa na kudorora kwa afya yake akisumbuliwa na shinikizo la damu.
Afya yake ilizidi kuwa mbaya, na hivyo akalazimika kurudishwa tena London Uingereza kwa matibabu.
Hata hivyo, Juni,1997, Kambona alifariki akipishana kwa siku chache tu na mdogo wake Otini Kambona ambaye pia alikuwa nchini humo kwa matibabu ya moyo.
Katika namna ambayo yaweza kuelezwa kuwa ni tendo pekee la kumuenzi mwanasiasa huyo mashuhuri, serikali ilikubali kusafirisha mwili wake na wa Otini na pia shughuli zote za mazishi.
Kambona ameacha mke na watoto wawili, akiwemo Neema Kambona ambaye hivi karibuni alijiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) tawi la London. Mtoto wa kwanza, Mosi Kambona aliuawa miaka si mingi sana iliyopita mjini London katika mazingira ya kutatanisha.
Kambona ameondoka, lakini pamoja na kuwepo kwa dosari hiyo ya kusigana katika siasa, alifanya makubwa mengi. Ni kiongozi pekee ambaye askari wa jeshi walipoasi na kuwalazimu Mwalimu Nyerere na Rashid Kawawa kukimbia, angeweza kutwaa madaraka ya nchi baada ya kufanya mazungumzo yaliyowalainisha wanajeshi hao.
Bila tamaa Kambona, alikwenda Kigamboni kuwachukua Mwalimu Nyerere na Kawawa waliokuwa mafichoni, na kubaki mwaminifu kwa nafasi yake ya uwaziri aliyokuwa nayo.
Kambona kasahaulika pamoja na uaminifu huo na mema yote kiasi kwamba hakuna hata sehemu ya kumbukumbu inayomwelezea kwa mazuri yake. Ameingizwa katika kapu la waliosahaulika!
Source: http://www.wavuti.com/#ixzz2KUyX6Sal --
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
0 Comments