[wanabidii] Oscar Kambona: Shujaa, Adui wa Taifa lake

Saturday, February 02, 2013
Oscar Kambona ni miongoni mwa viongozi mahiri na shupavu waliowahi
kuwa gumzo ndani na nje ya Tanzania, kutokana na uongozi wake, hekima
na busara.

Ndiye Mtanzania wa kwanza kuwa waziri aliyeongoza wizara mbili kwa
wakati mmoja. Ndiye Mtanzania pekee anayeaminika kusimama kidete na
kufanikiwa kulidhibiti jeshi lililoasi mwaka 1964.

Hata hivyo, pamoja na umahiri huo, lakini kubwa zaidi kutokuwa na
tamaa ya kutumia nafasi ya uasi wa jeshi kushika madaraka ya nchi.

Pamoja na hayo mchango wake hauthaminiwi kabisa. Tofauti na viongozi
wengine wa siasa au hata utamaduni, mpaka sasa hakuna barabara yenye
ukumbusho wa jina la mwanasiasa huyu aliyefariki akiwa katika matibabu
mjini London, Juni 1997 na mwili wake kurudishwa Tanzania kwa mazishi.

Oscar Kambona alizaliwa mwaka 1925, katika kijiji cha Kwambe kilichoko
mwambao mwa Ziwa Nyasa, karibu na
Mbamba-Bay, wilaya ya Mbinga, mkoani wa Ruvuma.

Alikuwa ni mtoto wa Kasisi David Kambona ambaye alikuwa miongoni mwa
Waafrika wa kwanza kupata upadri katika kanisa la Anglikana la
Tanganyika, na kwa mama Miriam Kambona.

Akiwa mdogo, baba yake alikuwa akimweleza kuhusu ndoto zake juu ya
uhuru wa nchi yake, hivyo kumfanya Oscar kujawa na hamu ya kuitumikia
nchi yake.

Msingi wa elimu yake aliupata nyumbani kwao, chini ya mwembe (ambao
bado uko mpaka sasa), katika kijiji cha Kwambe, kwa kuwatumia wazazi
wake wote wawili na mjomba wake, ambao wote walikuwa walimu.

Alipelekwa shule ya kati ya Mt. Barnabas, Liuli na baadaye Shule ya
Sekondari ya Alliance (sasa Shule ya Sekondari Mazengo), ambako
alilipiwa ada na askofu Mzungu wa Anglikana kwa vile baba yake
hakuweza kumudu kulipa ada ya pauni 30 kwa mwaka. Inasimuliwa kuwa
kilichomvutia Mzungu huyo kukubali kumlipia Oscar ada ni baada ya
kusali sala ya Baba Yetu Uliye Mbinguni kwa Kizungu.

Alichaguliwa kwenda 'Tabora Boys Senior Government School ambako ndiko
alikokutana na Mwalimu Julius Nyerere kwa mara ya kwanza. Wakati huo
Nyerere alikuwa anafundisha katika shule ya Kikatoliki ya St Marys.

Kukutana tena na Nyerere

Ilikuwa mwaka 1954, kwenye mkutano wa kitaifa wa walimu, ndipo Oscar
Kambona ambaye naye alikuwa amemaliza shule na kufundisha katika shule
ya Alliance, alikutana tena na Nyerere na kujadili mambo mbalimbali
ikiwemo harakati za chama cha TANU.

Oscar alishawishika kuitumikia TANU ambayo ilikuwa imeanzishwa muda si
mrefu, bila malipo baada ya Mwalimu Nyerere kumweleza kuwa asingeweza
kuajiriwa ndani ya chama kwa vile haikuwa na fedha.

Huo ulikuwa uamuzi mzito na mgumu mno, hasa kwa mtu kukubali kuachia
nafasi ya ualimu ambayo alikuwa akilipwa vizuri na kufanya kazi bila
malipo tena za chama ambacho ndiyo kwanza kilikuwa kikianza harakati
za ukombozi.

Kwa miezi takriban sita, Oscar Kambona alifanya kazi ngumu ya
kuzunguka sehemu mbalimbali za nchi na kuonana na machifu na wazee wa
vijiji ili kusajili wanachama.

Kwa kipindi hicho huku akitumia fedha kidogo alizokuwa amejiwekea
akiba yake, alifanikiwa kusajili wanachama 10,000 na haikuwa ajabu
kuwa baada ya mwaka mmoja alikuwa amepata wanachama hai 100,000.

Ili kutunza fedha za chama, Kambona alifungua akaunti ya kwanza ya
TANU na kisha kwenda Butiama kumshawishi Mwalimu Nyerere achukue
uongozi wa chama moja kwa moja kama mtendaji mkuu.

Mwaka 1957, Kambona alikwenda kusomea sheria katika Chuo cha Middle
Temple, nchini Uingereza kwa ufadhili wa Gavana.

Akiwa London Kambona alikuwa kiongozi wa chama cha wanafunzi wa
Tanganyika na mwenyekiti wa tawi la TANU la London.

Kukutana na watu mashuhuri

Mwaka 1958, Kambona alipata fursa ya kukutana kwa mara ya kwanza na
watu mashuhuri akiwemo George Padmore, mwanaharakati wa umoja wa wa
Waafrika duniani, ambaye alimshawishi ahudhurie mkutano wa Waafrika
wote (All Africa's Peoples Conference), uliofanyika nchini Ghana muda
mfupi baada ya kupata Uhuru.

Kambona alisafiri mpaka Ghana, wakati huo akiwa bado anaendelea na
masomo yake nchini Uingereza na huko alipata nafasi ya kukutana na
mwanaharakati mwingine maarufu wa siasa za Afrika, Kwame Nkrumah.

Utangazaji wake BBC

Kambona ndiye Mwafrika wa kwanza kutangaza taarifa ya habari kwa lugha
ya Kiswahili, katika Idhaa ya Kiswahili ya BBC, ambayo sasa
inajulikana kama (BBC Swahili).

Inadaiwa kuwa alikuwa akipenda sana uandishi wa habari kwenye vyombo
vya kimataifa.

Katika kuhakikisha anapigania uhuru na mafanikio ya TANU, Kambona
akiwa anaendelea na masomo yake nchini Uingereza, alikutana na Mwalimu
Nyerere kila alipoenda nchini humo na kupanga mikakati ya kudai uhuru.

Kambona alifunga ndoa na Flora Moriyo na harusi ilifungwa katika
kanisa la Mt. Paul, London, na Nyerere ndiye alikuwa msimamizi.

Kurudi Tanganyika

Mwaka 1959, Kambona alirudi Tanganyika na kuendeleza harakati za kudai
uhuru kupitia TANU, huku wakiweka bayana madai ya kupewa serikali ya
madaraka.

Kambona kwa kushirikiana na wenzake akiwamo Nyerere, waliweka mikakati
mbalimbali huku wakiwa tayari kuanzisha mapambano kama ilivyokuwa kwa
Mau Mau ya Kenya.

Katika uchaguzi wa kwanza TANU ilishinda viti vyote isipokuwa kimoja
na kuunda Serikali ya Mambo ya Ndani chini ya Mwalimu Nyerere ambaye
alikuwa Waziri Kiongozi wa kwanza.

Kambona aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na baadaye alishika nyadhifa
za Waziri wa Mambo ya Ndani, Mambo ya Nchi za Nje na Ulinzi na Tawala
za Mikoa.

Katika nyadhifa hizo, Kambona pia alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa
Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika na Mwenyekiti wa
Utayarishaji wa OAU ambayo sasa ni AU.

Kuunganisha bara na visiwani

Mwaka 1964, Kambona alifanya kazi kubwa katika kuunganisha Zanzibar na
Tanganyika, akiwa pamoja na Rais Nyerere na Karume. Hii ilikuwa ni
baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Januari 20, 1964, wanajeshi wa kikosi cha Calito waliasi. Kambona
akiwa waziri wa Ulinzi, alisimama kidete kusuluhisha na msemaji mkuu
upande wa serikali huku viongozi wakuu Mwalimu Nyerere na makamu wake,
Rashid Kawawa, ikisemekana wakiwa wamekimbilia mafichoni Kigamboni
walikokaa kwa siku tatu za majadiliano mazito mpaka machafuko
yalipoisha.

Moja ya nukuu za Kambona katika mahojiano na gazeti la Daily Telegraph
la London, alisema, "Baada ya kuwatuliza wanajeshi nilikwenda
kuwatafuta viongozi wengine na kuwarudisha mjini kwa kutumia Land
Rover yangu."

Kambona alisifiwa sana na Mwalimu Nyerere kwa hekima na busara yake
hadi kufanikiwa kumaliza uasi huo kwa kutumia nafasi yake ya uwaziri
wa ulinzi. Wapo walioanza kuvumisha kuwa huenda kwa uaminifu wake,
angeshika nafasi ya urais baada ya Nyerere kumaliza muda wake.

Ilikuwaje akawa adui wa serikali? Endelea toleo lijalo…

---
Imeandikwa na Andrew Chale/TANZANIA DAIMA


Source: http://www.wavuti.com/4/post/2013/02/oscar-kambona-shujaa-adui-wa-taifa-lake.html#ixzz2Jm5urm2n

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

0 Comments