[wanabidii] Karugendo amtabiria kifo Papa

Sunday, February 17, 2013
PAPA BENEDICT WA 16: Mfungwa wa imani anayetaka kuwa huru

Privatus Karugendo


KUTANGAZA kujiuzulu kwa Papa Benedict wa 16, kumewashutua wengi. Ni jambo ambalo sio la kawaida kwa kipindi cha zaidi ya miaka 600 hivi. Hadi sasa yamesemwa mengi na kila mtu ana mawazo yake.
Baadhi ya watu wameniomba nitoe mawazo yangu. Nilisita sana, maana sipendi kujiingiza kwenye malumbano ya kiimani. Watu wengi wanafikiri imani haijadiliki; mawazo ni kwamba tunaamini hata bila kufikiri!
Ingawa Papa Benedict wa 16, alisisitiza daima kwamba imani inaambatana na kufikiri, wengi hawapendi kukubali, na labda msimamo wake huo ndio umemponza.
Kwa vile watu wengi wameniomba nijadili mada hii, nitafanya hivyo bila kujiingiza kwenye malumbano ya kidini, lakini bila kupiga chenga ukweli kwamba imani inaambatana na kufikiri. Kuamini bila kufikiri ni matusi kwa Mwenyezi Mungu, aliyetuumba na akili na utashi.
Mwaka 1963, Kardinali Ratzinger (ndiye huyu Papa Benedict wa 16) alipokuwa na umri wa miaka 36, alimwandalia hotuba Kardinali Joseph Frings, Askofu Mkuu wa Cologne, kupinga msimamo mkali wa 'Congregation for the Doctrine of Faith' kwa kifupi C.D.F.
Miaka 19 baadaye, Ratzinger, ndie alikuwa kiongozi wa C.D.F, na kuwa na msimamo mkali zaidi ya waliomtangulia.
C.D.F ndiyo idara ya kulinda imani ya Kanisa Katoliki. Wakati ule ilikuwa na msimamo mkali hadi kuwachinja watu waliokuwa na mawazo tofauti na kanisa.
Hivyo Papa Benedict wa 16, wakati akiwa padri mdogo na mwanateolojia machachari, alipinga kwa nguvu zote idara hii ya kuisimamia na kuilinda imani ya Kanisa Katoliki.
Kwenye miaka ya sabini, Ratzinger alikuwa kati ya wanateolojia wanamapinduzi wa Ujerumani.
Huyu ndiye aliyewafundisha wanateolojia wa Latin Amerika, ambao waligeuka kuwa mwiba wa kanisa kwa kuanzisha teolojia ya ukombozi ambayo ilikuwa na mawazo kwamba kanisa ni lazima lifanane na ujumbe wake wa kuwakomboa masikini, wanyonge na wanaonewa. Na kwamba madaraka ya Kanisa Katoliki ni lazima yatoke chini kwenda juu, si kutoja juu kwenda chini.
Maana yake ni kwamba, madaraka yaanzie kwenye jumuiya ndogo ndogo. Mapadre, maaskofu, wachaguliwe kutoka kwenye jumuiya ndogo ndogo, na wapate madaraka yao kutoka kwenye jumuiya hizo na wala sio kutoka Roma.
Wanateolojia hawa walianza kuhoji ni kwanini kanisa katika nchi zao lilikuwa upande wa serikali na matajiri, badala ya kuwa upande wa wananchi wanyonge?
Wakaanza kujiunga na makundi ya wapigania uhuru kwenye nchi zao na kuingia msituni kupigana bega kwa bega na wananchi waliokuwa wakipinga ukandamizwaji wa serikali zao.
Roma, ikawa upande wa serikali na kupingana na hao mapadri wa teolojia ya ukombozi.
Teolojia ya ukombozi ilipoanza kushika kasi na kuaminika kwamba ilichochewa na wanafunzi wa Ratzinger kama vile Padri Leonardo Boff kutoka Brazil, Ratzinger alianza kurudi nyuma kidogo.
Alipoanza kuonesha dalili za kutofautiana nao, Hans Küng, mwanateolojia mwingine mwanamapinduzi wa Ujerumani alimtania: "Ukitaka kuwa kardinali katika nchi ya Ujerumani, ni lazima kuanza mapema kufanya mazoezi ya kuwa mfungwa wa imani."
Alipochaguliwa kuwa kardinali mwaka 1977, Küng, alimkumbusha maneno hayo. Na alipoteuliwa kuwa Papa Benedict wa 16, maneno hayo yakawa yametimia, maana mapapa wote ni wafungwa wa imani!
Mfungwa wa imani, anakuwa hana tena ule uhuru wa kutoa maoni yake mwenyewe, anakuwa hana tena uhuru wa kujadili na kuhakikisha anakubaliana na nafsi yake. Analindwa na kuongozwa na chombo cha uongozi wa kanisa; hivyo mawazo yake ni lazima yapimwe na kupitiwa na watu mbali mbali.
Huko nyuma, mapapa walikuwa ni wafungwa ndani ya Vatican; hawakutoka nje au kutembea nchi za nje, walikaa ndani na kupata habari juu ya dunia inayowazunguka kupitia chombo cha uongozi wa kanisa. Hivyo waliyajua yale tu ambayo chombo cha uongozi wa kanisa kilitaka wayajue.
Mfungwa wa imani hawezi kuwa huru. Huu ndio uongozi wa Kanisa Katoliki. Uhuru wa mfungwa wa imani ni kifo. Historia inatuonesha kwamba mapapa wote waliotaka kuwa huru, hawakupona!
Na miaka ya hivi karibuni, dunia ilishuhudia kifo cha Papa John Paul I, aliyetaka kuwa huru ndani ya siku 33 za utawala wake. Kwa vile alitaka kuwa huru, hakuendelea kuishi. Ili uwe Papa ni lazima uwe mfungwa wa imani.
Ufungwa wa imani ndani ya Kanisa Katoliki unaanzia kwa ngazi ya askofu na makardinali. Hawa wote ni wafungwa wa imani. Swali la kujiuliza je, Kardinali Ratzinger alikubali kuwa mfungwa wa imani?
Oktoba 1, 1986 Kardinali Ratzinger, alitoa mwongozo wa Kanisa Katoliki juu ya watu wanaovutiwa na jinsia zao (homosexuality).
Mwongozo huu ulikuwa ni barua aliyowaandikia maaskofu wote wa Kanisa Katoliki: "On the pastoral care of homosexuals".
Katika barua hii, Kardinali Ratzinger aliwakumbusha maaskofu juu ya mwongozo mwingine kuhusu suala hili hili uliotolewa Desemba 1975 - "Declaration of Certain Questions Concerning Sexual Ethics" uliosisitiza kwamba hali ya mtu kuvutiwa na jinsia yake ifanyiwe utafiti na ichukuliwe kwa uangalifu na busara.
Katika barua hiyo Kardinali Ratzinger, aliwashauri maaskofu kwamba hali ya mtu kuvutiwa na jinsia yake inahitaji wachungaji (mapadri) wenye kufanya utafiti kwa uangalifu mkubwa, wenye kujali, wa kweli na wenye teolojia isiyokuwa ya msimamo mkali.
Ingawa Kadinali Ratzinger, anapinga hali hii na kuiona kama hali fulani ya ugonjwa na kufanya mambo kinyume na maumbile, anashauri watu wenye matatizo ya kuvutiwa na jinsia zao wasitengwe.
Wapatiwe huduma za kiroho, washauriwe na kuvumiliwa hadi pale watakapobadilika. Anasema wachukue njia ya msalaba. Wakubali kuwekwa msalabani na kufa na kufufuka kama alivyofanya Yesu Kristu. Wazaliwe upya na kupata maisha mapya.
Anakubali kwamba ni kitu kigumu mtu kuachana na tabia yake aliyozaliwa nayo, lakini hiyo ndiyo njia ya msalaba. Si jinsi mtu anavyotaka yeye, bali ni jinsi anavyotaka Mwenyezi Mungu!
Kwa wachambuzi, msimamo kama huu sio wa mfungwa wa imani; mawazo binafsi ya Ratzinger yalipenyeza sana kwenye waraka huu. Na aliendelea kuandika vitabu na kukutana na wanafunzi wake na kuendeleza mijadala kiteolojia.
Ukikutana naye kwa faragha, unaweza kujadiliana nae juu ya uzazi wa mpango, kutoa mimba, kuwapadrisha wanawake, kupunguza madaraka ya Roma. Atakusikiliza, atachangia, lakini akisimama kama 'mfungwa wa imani'.
Kama alivyokuwa kardinali msimamizi wa imani ya Kanisa Katoliki, hana huruma kutumia nyundo yake kwa nguvu zote kuwasambaratisha wenye mawazo ya kutishia uhai wa imani ya Kanisa Katoliki, hata kama mawazo hayo alikuwa akiyakubali faraghani.
Mwaka 1985, alimnyamazisha bila huruma mwanafunzi wake, Padri Leonardo Boff, kutoka Brazil.
Kumpatia upapa, ilikuwa ni hatua ya kumzima zaidi, maana alitaka kuachia ngazi ya ulinzi wa imani, kabla ya kifo cha Papa John Paul II, ili aandike vitabu. Alikataliwa, akaombwa aendelee na baada ya kifo cha Papa John Paul II, akateuliwa kuwa Papa.
Hata hivyo aliendelea kuandika. Na kama mnakumbuka kitabu chake cha mwisho ni 'Yesu wa Nazareti' na hoja kwamba miaka inayotajwa kwenye Biblia ya kuzaliwa kwa Yesu, ni uongo. Na akaenda mbali kuruhusu matumizi ya kondomu kwa wanandoa ambao mmoja wao ana virusi.
Ukisoma kitabu hicho, utagundua kwamba mtu ambaye kanisa lilikuwa na nia ya kuzima mawazo yake kwa kumpatia madaraka ya juu, alianza kuvunja kuta na kutaka kuwa huru.
Kanisa Katoliki ni taasisi na lina wenyewe ambao kwa kiasi kikubwa hawataki mambo yabadilike. Hivyo ili kuliongoza ni lazima ukubali kuwa mfungwa katika imani.
Hivyo inawezekana kabisa, Papa Benedict wa 16, ameshinikizwa kuachia ngazi baada ya kugundua kwamba hawawezi kumzima na nafasi yake ni kubwa kwa kuweza kufanya chochote na akasikilizwa.
Kama ni shinikizo, basi atakuwa amewazidi kete walinzi wake, maana uamuzi wake aliuficha na kuutoa hadharani. Hili limewachukiza wakubwa hao, na wengine wanataka aondoke haraka kwenye mji wa Roma, maana ni aibu Papa kujiuzulu.
Papa, anayejulikana kujiuzulu alifia gerezani! Lakini pia, kufuatana na uanamapinduzi wake, inawezekana kaamua kuachia ngazi mwenyewe. Anataka kuwa huru! Ni imani yangu kwamba anajua kabisa kwamba uhuru wa mfungwa wa imani ni kifo!

Share this :

Related Posts

0 Comments