WANABIDII,
Hebu angalieni utafiti wangu kisha naomba maoni yenu.
Niliamua kufanya utafiti wa KUTAKA kujua kiasi ambacho askari wetu hutoza kama rushwa (Bakshishi, tip under the table etc...) kwenye vituo ambavyo hutumia CAMERA maalumu za kupimia kasi ya magari. kama tochi zinazotumika na askari TRAFIKI kupimia kasi ya magari ziko sahihi. Sintaweza kusema hapa kwamba utafiti huu ulifanyika wapi na barabara gani kwa ajili ya usalama wa watumishi hao wenyewe kwa kuwa sikuona kosa lolote kwao.
Matokeo yake yamenistua sana kwa kuwa yamekuwa tufauti na nilichotegemea kupata na kuja na matokeo mengine ambayo pia yalinichanganya.
Siku ya kupima ukweli huu tuliamua kutumia magari manne tofauti tukiwa madereva watatu na dereva wa nne wa kukodisha yeye bila kujua kinachoendelea. Mipango yote ilienda vizuri kama ilivyopangwa kuanzia maandalizi hadi utekelezaji.
Dereva wa kwanza nilikuwa mimi mwenyewe. Kwanza nilipita mimi kwenye kituo cha Polisi nikiwa na kasi ya 55 - 60kph, nilikamatwa na kuoneshwa nyuma ya CAMERA kuwa nilikuwa natembea kwa kasi ya 63kph. Sikuombwa rushwa ila nililipa faini 30,000.00 pamoja na kujitetea ili kuweka mazingira ya kuombwa chochote hawakukubali nikalipa faini.
Kisha mwenzangu wa pili alifuatia ambaye tulikubaliana kuachiana umbali wa robo saa kila mmoja ili kupoteza lengo kama mtu angeweza kuhisi au kutufahamu kwa majina na sura. Yeye alikuwa akitembea kwa kasi ya 65 – 70kph alipokuwa akiingia sehemu walipo POLISI, yeye aliambiwa ana kosa la kwenda kasi kwa mwendo wa kilometa 61kph. Hakuombwa rushwa ila alilipa shs: 30,000.00 aliweka mazingira mazuri lakini hakuombwa.
Kisha akaja rafiki yetu wa tatu ambaye tulikubaliana aingie katika eneo hilo la POLISI kwa mwendo kasi wa 70 – 80kph, alipokamtwa aliambia anatembea kwa mwendo kasi wa 65kph. Hakuombwa rushwa ila aliandikiwa kulipa shs: 30,000.00 ambazo hakulipa siku hiyo hiyo isipokuwa keshoyake. Jitihada ilikuwa ni kuweka mazingira ya kuombwa rushwa lakini hakuombwa.
Mwishoni tuliamua wote watatu kuingia gari moja tukiwa tumebadilisha mavazi na kuvaa kofia za kapelo ili kujaribu kuficha sura zetu tusitambulike kwa urahisi. Tulimkodisha dereva mwingine ambaye hatukutaka ajue kinachoendelea. Yeye tulimwambia tunawahi mahali Fulani kwa hiyo atuwahishe. Alitoa tahadhali ya uwepo wa polisi, lakini tulimwambia tutalipa faini yeye atuwahishe tu, alikataa kasha tukakubaliana aendeshe kwa mwendo wa kati ya 50 – 55kph. Tulipofika katika kituo hicho tukasimamishwa na kuambiwa tunakwenda kwa kasi ya 58kph. Hatukuombwa rushwa na wala hatukulipa faini. Tulionywa.
Matokeo haya ya vipimo tofauti kwa tochi moja ambayo inayotumiwa na mtu mmoja tu yalifanya tubaki na maswali haya yafuatayo: -
1. Tochi hizi ni mbovu kutokea zilipotengenezwa hivyo kama madereva wataamua kubishia kasi wanayosomewa wanaweza kushinda kesi zao mahakamni.
2. Vipimia kasi vya magari yetu huenda vilipata matatizo japokuwa tulitengeneza kwanza kabla ya kuanza utafiti huu.
3. Tochi hizi ni nzima lakini huenda watumiaji hawajui jinsi ya kuzitumia. Hatujachukua jukumu la kuwauliza kama POLISI hawa walipata mafunzo ya kuzitumia.
Mtizamo wangu ni kuendelea na utafiti huu mahali pengine ili kujua hasa ni kiasi gani watu wanaombwa wawapo barabarani kama madereva kwa kuwa malalamiko haya bado yapo..
Lakini je katika matokeo haya WANABIDII ninyi mnasemaje?
Kunyaranyara, E.M.S.
0 Comments