Hivi ile asasi iliyoanzishwa na Mama Anna Mkapa iliyokuwa ikiitwa kwa jina la EOTF (Equal Opportunity for all Trust Fund) ilifia wapi? Mbona siku hizi asasi ile haisikiki? Na sio asasi pekee isiyosikika, bali hata Mkurugenzi wake (Mama Anna Ben) naye haonekani na wala hasikiki kabisa. Hivi mama huyu bado yupo nchi hii au kalihama jiji? Yawezekana ama asasi yake ilikufa au aliihamishia nchi nyingine (aliyohamia?). Vinginevyo, nashawishika kuamini kwamba asasi ile ilisajiliwa kufanya kazi kwa kipindi cha miaka 5 au 10, na kwamba baada ya muda huo kuisha, asasi nayo ikafa.
Inavyoonekana ni kwamba tabia hii ya wake za marais kuanzisha asasi pindi waume zao wanapokuwa ikulu imeanza kuwa jambo linalozoeleka taratibu. Mara baada ya rais JK kuingia ikulu, Mama JK naye akamuiga Mama AnBen kwa kuanzisha taasisi ya WAMA (WAnawake na MAendeleo). Nadhani hizi asasi zinakuwa ni kama 'mashine' za kukamulia pesa za wafadhili kwa kisingizio cha kusaidia wananchi maskini. Hizi ni taasisi ambazo hutumiwa na hawa First Ladies kama makapu ya kuhifadhia pesa za kufanyia shopping ndani na nje ya nchi.
Wasiwasi mwingine ni kwamba baadhi ya asasi hizi zinaweza kutumika kama lango au kipengere cha kupitishia hongo au rushwa, hata kutafuta umaarufu na upendeleo wa aina fulani.
Kama kweli hizi taasisi zingekuwa na malengo chanya ya kusaidia 'masikini', badala ya kutumiwa kama makapu ya kuhifadhia pesa za kufanyia shopping kwa first ladies, zisingekuwa 'zinakufa' mara baada ya waume zao kuondoka ikulu. Tafakari, chukua hatua!
0 Comments