[wanabidii] Mifuko Ya Hifadhi Ya Jamii Iwe Chini Ya Wizara Moja

Monday, November 05, 2012

Mwanzoni mwa mwezi huu Mfuko wa Pensheni wa PPF uliandaa Mkutano wa Wanachama na Wadau wake mjini Arusha ukiwakutanisha zaidi ya washiriki 500 kutoka ndani na nje ya nchi. Mada nyingi zilijadiliwa, haya ndiyo Mwandishi Wetu aliyokusanya.

SERIKALI iangalie uwezekano wa Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii kusimamiwa na wizara moja ili kurahisisha uratibu, ni kati ya maazimio yaliyopitishwa mwezi huu katika Mkutano wa mwaka wa Wanachama wa Mfuko wa Pensheni wa PPF uliofanyika Arusha.

Kwa sasa Mifuko hiyo husimamiwa na wizara mbalimbali zikiwamo za Kazi, Fedha, Afya na Tawala za Mikoa, hali hiyo ikielezwa kwamba inasababisha uratibu kuwa mgumu.

Maazimio mengine ya wanachama hao, yanayotakiwa yafanyiwe kazi kuanzia mwaka huu ili majibu yake yapatikane kabla ya mkutano mwingine Oktoba mwakani, ni pamoja na waajiri watoe fursa maalumu kwa wawakilishi wao walioshiriki katika mkutano wa mwaka huu kukutana na wafanyakazi wenzao ili kutoa taarifa ya yaliyojadiliwa na maazimio.

Aidha, wanachama na wadau hao wametaka PPF, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kuongeza utoaji elimu kwa umma juu ya dhana nzima ya pensheni ili, pamoja na mambo mengine, wanachama waweze kufahamu haki na wajibu wao.

Azimio jingine ni linalohusiana na fao la elimu kwamba PPF iendelee kufanya utafiti kuhusu namna ya kuliboresha fao hilo ili watoto wa wanachama wanaofariki wakiwa kazini walipiwe gharama za masomo yao hadi kidato cha sita.

Mengine ni PPF itangaze zaidi Mfumo wa Amana (Deposit Administration Scheme) ili kuvutia watu wengi kujiunga na mfumo huo na hivyo kuongeza idadi ya wanachama; ielimishe zaidi wanachama na umma jinsi ya kutumia teknohama katika kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na Mfuko ; SSRA iongeze kasi ya kuoanisha na hatimaye kutangaza fomula mpya ya kukokotoa mafao ya pensheni kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Serikali iangalie uwezekano wa kutoza asilimia ya mapato yatakayotokana na uchimbaji wa gesi asilia na mafuta kuanzisha Mfumo wa Hifadhi ya Jamii kwa Wote (Universal Social Protection) na waajiri waelimishe wafanyakazi wao kuhusu mitindo ya maisha (healthy life styles) na aina ya vyakula vinavyopunguza uwezekano wa kupata magonjwa kama vile saratani, kisukari na shinikizo la damu.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio aliwaambia wanachama na wadau kwamba Mfuko umeendelea na juhudi za kusogeza huduma karibu na wateja kwa kuendelea na matayarisho ya ufunguzi wa Ofisi ya Kanda ya Kusini katika Manispaa ya Mtwara na ofisi za uwakilishi katika Manispaa za Tabora na Moshi.

Mfuko tayari una ofisi nyingine za Kanda za Kinondoni, Ilala na Temeke jijini Dar es Salaam, Kanda ya Mashariki na Kati katika Manispaa ya Morogoro, Kanda ya Kaskazini katika Jiji la Arusha, Kanda ya Ziwa katika Jiji la Mwanza na Nyanda za Juu Kusini jijini Mbeya.

Erio alisema pia kwamba Mfumo wa PPF Taarifa umeendelea kufanya kazi vizuri, kwamba mwanachama anaweza kuingia katika mfumo huo na kupata taarifa zake za michango, madai ya mafao na malipo ya pensheni kwa kutumia simu za mkononi na kompyuta.

Akizungumzia mafao, Erio alisema malipo ya pensheni na mafao mengine yaliongezeka kwa asilimia 12.6 kutoka shilingi bilioni 63.5 kwa mwaka 2010 hadi kufikia shilingi bilion 71.88 kwa mwaka 2011 na kwamba kuanzia mwaka 2008, PPF iliteuliwa kuwa wakala wa Serikali katika kuwalipa wastaafu wa Serikali na imeendelea na jukumu hilo ikilipa kiasi cha shilingi bilioni 69.6 kwa wastaafu 58,603 wa Serikali.

Alisema pia kwamba kutokana na utendaji mzuri wa Mfuko, thamani ya Mfuko iliongezeka kwa asilimia 23.8 kutoka shilingi bilioni 722.47 Desemba 2010 hadi shilingi bilioni 894.52 Desemba 2011, huku idadi ya wanachama wa Mfuko ikifikia wanachama 180,049 mwishoni mwa mwezi Desemba 2011.

Kuhusu uandikishaji wanachama na ukusanyaji michango, alisema Mfuko umeendelea kutoa taarifa za michango kwa wanachama wake na kuimarisha uwezo wake wa kuuza shughuli za Mfuko katika ofisi zake za Kanda kwa nia ya kuandikisha wanachama wapya.

Juhudi na mikakati hiyo imewezesha Mfuko kuandikisha wanachama wapya 59,217 kwa mwaka 2011 ikilinganishwa na wanachama 40,735 kwa mwaka 2010.

Aidha, alisema makusanyo yatokanayo na michango yaliongezeka kwa asilimia 27 kutoka shilingi bilioni 147.6 mwaka 2010 hadi kufikia shilingi bilioni 187.5 mwaka 2011. Hii ilichangiwa na kuongezeka kwa mishahara na kuandikishwa kwa wanachama wapya.

Kuhusu uwekezaji, alisema Mfuko uliendelea kuwekeza katika maeneo manne ya mali zenye faida inayojulikana kabla ya kuwekeza, hisa za makampuni, majengo, na mfuko wa uwekezaji wa pamoja. Jumla ya uwekezaji kwa mwaka 2011 ulikuwa shilingi bilioni 835.8 ambao uliuletea Mfuko mapato ya shilingi bilioni 91.4.

Akizungumzia changamoto alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana mwaka 2011, kulikuwa na changamoto kadhaa zilizoukabili Mfuko. Hizo ni kushuka kwa riba katika amana za uwekezaji, ufinyu wa wigo wa uwekezaji, kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania, madai ya wanachama kuoanisha fomula ya pensheni, na ushindani usiofuata taratibu za kisheria katika kuandikisha wanachama.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, alisema Mfuko utahakikisha kuwa vitega uchumi vingine vinatafutwa katika majengo, hisa na vipande vya dhamana ili kutatua tatizo la ushukaji wa mapato katika soko la fedha. Mfuko pia utaiomba SSRA kuhakikisha kanuni ya kukokotoa mafao ya pensheni inaoainishwa na kunakuwapo na uendelezaji wa uanachama pale inapotokea mwanachama anabadilisha mwajiri.

Kwa kawaida mkutano huo wa wanachama na wadau hujadili na kusikiliza mada mbalimbali. Kati ya mada zilizowasilishwa na kusisimua safari hii ni iliyohusu maandalizi ya kuelekea kustaafu.

Je, umepata kujiuliza utaendeshaje maisha yako baada ya kustaafu kama Mwenyezi Mungu atakuwa ameendelea kukuweka hai?

Utamudu vipi kuendesha familia yako katika hali ambayo hautakuwa mwajiriwa katika maisha ya leo ambayo yamepanda sana?

Hivi tunajua kwamba kuna maisha baada ya kustaafu ambayo tutayahitaji na hivyo inatubidi tujiandae ili tuendelee kufurahia uhai sisi na wategemezi wetu?

Tumepata kusikia ndugu na jamaa waliotangulia mbele ya haki mara tu baada ya kustaafu? Na hao si ndio waliokuwa wakiishi vizuri katika nyumba za mashirika na taasisi mbalimbali, zikiwa na kila kitu cha kisasa?

Umepata kufikiria msongo wa mawazo utakaokukumba wewe na wanafamilia wako pale utakapoambiwa ghafla kwamba kibarua chako kimeota nyasi na hivyo unapaswa kuachia nyumba na mali za shirika ndani ya miezi mitatu huku ukiwa huna pa kwenda?

Hayo na maswali mengi lukuki ndiyo ambayo Juma Muhimbi, mfanyakazi wa zamani wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, ambaye alistaafu na sasa ni mjasiriamali, alikuwa akiyatafakari na wajumbe wengine alipowasilisha mada hiyo ya mandalizi kabla ya kustaafu.

Alisema Muhimbi: " Hayo ndiyo ambayo huwafanya baadhi ya wastaafu ama kufariki dunia au kudhoofika muda mfupi baada ya kustaafu kwa vile wengi wanakuwa hawakujiandaa kustaafu."

Aliongeza Muhimbi: " Ni kwa ajili ya mambo kama hayo yaliyomfanya Malcolme S Forbes kusema haya yafuatayo, "kustaafu huua watu wengi zaidi ya kazi ngumu ilivyopata kuua".

Alisema kwamba mmoja wa wandishi wa vitabu akizungumzia maisha ya kustaafu, alipata kusema: " Muda mzuri wa kuanza kufikiria kustaafu ni kabla ya bosi wako hajaanza kuwaza kwamba unapaswa kustaafu".

Alisema ni muhimu kwamba kila mwajiriwa awe anapanga maisha yake kabla ya kustaafu ili ikitokea akastaafu basi muda huo umkute akiwa ametulia kifikra.

Kwa mujibu wa Muhimbi, kujiandaa kustaafu si suala dogo, na wengi hukwaza na jinsi gani watapanga maisha yao wanapokuwa wanataka kufanya hivyo kabla ya kustaafu.

"Wengi wanashindwa jinsi ya kuanza kupanga maisha yao kabla ya kustaafu, tatizo ni je, jinsi gani wanaanza kujiandaa? Wala hakuna haja ya kuanza kudokoa huku na kule kwa kisingizio cha maandalizi ya kustaafu," alisema.

Umuhimu wa maandalizi ya kustaafu

Kwa mujibu wa Muhimbi haifai kustaafu ghafla kwa vile kufanya hivyo kuna madhara ya kisaikolojia, madhara ya kimwili na hata ya kijamii.

Alisema dhana ya kustaafu imejikita katika ukweli kwamba maisha ya ustaafu yanatakiwa yaendeshwe kwa vyanzo mbalimbali vya mapato vikiwamo pensheni na akiba ambazo mstaafu alijiwekea wakati akiwa katika ajira.

Hiyo ni kutokana na kwamba kustaafu hakumfanyi mstaafu kuachana na matumizi ya msingi aliyokuwa nayo wakati akiwa katika ajira.

Alisema Muhimbi: " Japo inawezakena kwamba kazi ikakoma baada ya mtu kustaafu, maisha lazima yaendelee, hivyo mstaafu bado atahitaji kula, kuishi na kujichanganya na watu wengine, na hayo yote yana gharama. Ni kwa ajili hii kwamba mtu anapaswa kujiwekea akiba ili anapostaafu awe na kipato cha kumuwezesha kumudu baadhi ya gharama za maisha.

" Haitoshi tu kufikiria ni akiba kiasi gani unayo, bali ni muhimu pia kuweka muundo wa jinsi mstaafu anavyopenda kuishi baada ya kustaafu. Hii itasaidia kupima ni kiasi gani cha kipato unachokihitaji kwa maisha yaliyosalia."

Uzoefu binafsi wa mstaafu

Muhimbi alistaafu Mei mwaka 2001 akiwa na umri wa miaka 47 kutokana na sababu alizosema zilikuwa nje ya uwezo wake. Alisema wakati huo hakuwa amejiandaa kustaafu kutokana na ukweli kwamba hata umri wa hiari wa kustaafu wa miaka 55 alikuwa hajautimiza.

" Nilikuwa na kazi iliyokuwa inalipa vizuri. Nilikuwa naishi kwenye nyumba nzuri ya shirika iliyokuwa na kila kitu. Lakini nilitakiwa nihame ndani ya miezi mitatu. Japo nililipwa nauli ya kwetu, Kwachaga, Handeni, sikuwa na mpango wa kwenda huko. Hakika hii ilikuwa ni changamoto kubwa kuendelea kuishi Dar es Salaam," alisema Muhimbi.

Yote kwa yote, leo miaka 11 baadaye Muhimbi bado anadunda, tena anaonekana mambo yake ni mazuri, sasa akiwa mjumbe bodi na akiendesha shughuli mbalimbali za kitaalamu za uhasibu zinazomlipa vyema.

Anasema kati ya mambo yaliyomsadia ni kwamba kwa muda wote wa ajira alikuwa mwanachama wa PPF (kwa miaka 21) ingawa katika muda huo alikuwa amebadili waajiri. Hiyo maana yake ni kwamba alikuwa akilipwa mafao mazuri ya kustaafu.

Anasema changamoto ilikuja pale mwaka 2002 PPF ilipositisha kumlipa mafao ya kila mwezi kutokana na mabadiliko ya sheria yaliyokuwa yanasisitiza walipwe tu wale waliokwishakutimiza miaka 55.

" Desemba 2002 PPF ilisimamisha kulipa penshen za kila mwezi kwa wastaafu wote waliokuwa chini ya miaka 55. Hilo lilikuwa fundisho jingine, kwamba hata ndani ya ustaafu lazima uwe unapangilia mambo yako," alisema.

Anawashauri vipi wastaafu watarajiwa? Ni muhimu kuandaa mapema jinsi ya kustaafu na mtu asisubiri mpaka wakati wa kustaafu unapowadia kuanza maandalizi. Mtu asisubiri kujianda wakati tayari kishagonga miaka 50.

Mifuko ya Jamii inasaidia wakati wa kustaafu lakini hilo ni eneo moja tu, mipango ya kustaafu ilenge pia maeneo mengine ya kuongeza kipato. Kikubwa mtu asiguse mafao yake hata kama atakuwa anabadili ajira kila mara.


Makala hii imenukuliwa kutoka kwenye gazeti la RaiaMwema, toleo la 266.

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

Share this :

Related Posts

0 Comments