[wanabidii] Ufafanuzi wa Wizara Kuhusu Kuuzwa kwa Hisa za Kampuni ya TanzaniteOne.

Saturday, December 13, 2014
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 

WIZARA YA NISHATI NA MADINI

TAARIFA KWA UMMA

Ufafanuzi Kuhusu Kuuzwa kwa Hisa za Kampuni ya TanzaniteOne.

Gazeti la Raia Mwema la Desemba 10, 2014 liliandika habari iliyodai kwamba mmoja wa Wafanyabishara maarufu wa mjini Arusha alishirikiana na mtoto wa kiongozi wa juu wa Serikali na vigogo wa Wizara ya Nishati na Madini kufanikisha uuzwaji wa asilimia 50 ya hisa za Kampuni ya Richland Resources katika Kampuni ya TanzaniteOne inayochimba madini ya Tanzanite katika eneo la Merelani Wilayani Simanjiro.

Aidha, taarifa hiyo ilidai kuwa licha ya hisa hizo kuuzwa kwa mamilioni ya Dola, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya TanzaniteOne ametoa taarifa kuwa hisa hizo zimeuzwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani 5.1milioni (sawa na shilingi bilioni 8.8 za Kitanzania) ili kukwepa kodi. Vilevile, taarifa hiyo imeeleza kuwa Wizara ina ukiritimba wa kuwawezesha watanzania kumiliki rasilimali na kwamba leseni ya TanzaniteOne ilitolewa kimakosa na hivyo si halali. 

Wizara inapenda kutoa maelezo yafuatayo kuhusu hoja zilizotolewa:

Suala la Uuzaji wa Hisa za TanzaniteOne

Kampuni ya TanzaniteOne imeijulisha Wizara kuhusu kusudio la kuuza hisa zake asilimia 50 kwa Kampuni ya Sky Associate Group Limited. Kampuni ya TanzaniteOne haijaomba rasmi Wizara iridhie uuzaji wa hisa zinazokusudiwa kuuzwa. Mara Kampuni hiyo itakapowasilisha taarifa kamili za kuuza hisa zake ikiambatana na maombi ya kupata ridhaa ya kuhamisha umiliki wa hisa hizo kwa Kampuni ya Sky Associates Group Limited, Wizara itafanya uchunguzi wa kina na kuona kama utaratibu umefuatwa wakati wa kuuza hisa hizo. 

Uhalali wa Leseni ya TanzaniteOne/STAMICO
Kampuni ya TanzaniteOne imekuwa ikimiliki leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini-Special Mining Licence (SML 8/92) kwa asilimia 100 katika eneo la Kitalu C Merelani iliyotolewa mwaka 1992. Leseni hiyo ilikuwa inafikia ukomo wake tarehe 9 Julai, 2012. Tarehe 25 Januari, 2011 Kampuni ya TanzaniteOne iliwasilisha ombi la kuhuisha leseni hiyo kwa lengo la kuendelea kuchimba madini katika eneo hilo la Kitalu C. 

Wizara ilielekeza Kampuni ya TanzaniteOne irekebishe ombi la tarehe 25 Januari 2011 kwa mujibu wa Kifungu cha 116 cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Kifungu hicho kinaruhusu kufanyika marekebisho mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha leseni zilizotolewa chini ya Sheria ya Madini ya Mwaka 1998 kuhamia kwenye Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Marekebisho kama hayo yamefanywa kwa maombi ya leseni za utafutaji mkubwa wa awali wa madini (PLR) na leseni za uchimbaji madini ya vito (GML) ambazo hazitolewi tena chini ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. 

kwa kuwa Kampuni ya TanzaniteOne ilikwishamilikishwa leseni katika eneo hilo kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 1998, uhuishaji wa leseni Na. SML/8/92 na marekebisho yaliyofanyika haukufanywa kwa mujibu wa Kifungu cha 8 cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, bali chini ya kifungu cha 116 kama ilivyoelezwa awali.

Kwa kuwa maombi ya Kampuni ya TanzaniteOne yalishughulikiwa katika mazingira ya kufanya marekebisho (modification) ya leseni kutoka Sheria ya Madini ya Mwaka 1998 kwenda katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, leseni mpya (ML 490/2013 )ilitolewa kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya Tanzanite, tsavorite, graphite na madini mengine yanayoweza kupatikana. Leseni hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 7.6. Kihistoria uchimbaji katika kitalu C umekuwa ukihusisha madini hayo yaliyoainishwa katika leseni hiyo.

Katika miaka ya 1970, TGI walijihusisha zaidi na uchimbaji wa madini ya vito. Baadaye miaka ya 1990, Kampuni ya Graphtan Ltd ilijihusisha zaidi na uchimbaji wa graphite katika eneo la kitalu C, huku madini ya vito (Tanzanite) yakiwa ni by-product.

Kwa kuzingatia matakwa ya Sera ya Madini ya Mwaka 2009 yanayohusu ushiriki wa Serikali kimkakati katika miradi ya madini, Serikali ilifanya majadiliano na Kampuni ya TanzaniteOne yaliyowezesha STAMICO kumiliki asilimia 50 ya hisa katika mgodi huo wa Tanzanite. Kutokana na makubaliano hayo Kampuni ya TanzaniteOne ilifanyia marekebisho ombi lake la leseni ya uchimbaji madini na kuingiza STAMICO ambayo inamiliki asilimia 50 katika leseni ya uchimbaji madini eneo la Kitalu C.

Uwezeshaji wa Wazawa katika Sekta ya Madini

Katika taarifa ya gazeti hilo la Raia Mwema ilidaiwa kuwa Wizara ya Nishati na Madini ina ukiritimba uliokithiri na viongozi wake hawatoi fursa kiuwezeshaji kwa wazawa katika sekta ya madini.

Madai hayo ni kupotosha ukweli kwamba Wizara imepiga hatua kubwa katika urasimishaji leseni kwa watanzania na katika uwezeshaji wa wachimbaji wadogo. Hadi sasa kati ya leseni za madini zipatazo 45,000, Watanzania wanamiliki asilimia 75 ya leseni zote, na wageni wanamiliki asilimia 25. Aidha, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2011/12 hadi sasa Wizara imetenga maeneo 33 kwa ajili ya uchimbaji mdogo; pamoja na kutenga takriban shilingi bilioni 8 kwa ajili ya uwezeshaji wa wachimbaji wadogo kupitia Benki ya Maendeleo ya TIB.

Imetolewa na,

WIZARA YA NISHATI NA MADINI

11 Desemba, 2014

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments