[Mabadiliko] SULUHISHO LA KURA YA WAZI AU SIRI

Monday, March 10, 2014
 
Kabla ya kuwasilisha hoja yangu, naomba ieleweke wazi kwamba ninao uhuru kutumia wahusika hai, waliohaishwa au waliohuishwa ktk kuwasilisha hoja yangu. Hili ni suala ambalo linakubalika kisarufi na kimuundo.
 
Napenda kuchukua fursa hii kuwaomba wajumbe wote wa bunge la katiba wakubali ipigwe kura ya SIRI na wajumbe wote ili kufikia uamuzi wa ama kutumia kura ya wazi au siri katika kupitisha vifungu vya katiba kwani, kwa jinsi hali ilivyo, sio rahisi kufikia muafaka kufuatia mvutano wa kimakundi uliopo. Kundi kubwa linataka kura ya wazi na kundi dogo linataka ipigwe kura ya siri, kama ilivyozoeleka kisheria.
 
Kinadharia, kundi kubwa lina advantage kwa uamuzi wowote utakaofikiwa kwa kuwa lina wajumbe wengi pia. Hata kama ikiamuliwa ipigiwe kura ya siri kuamua matumizi ya kura ya wazi au siri, ni dhahiri kwamba kundi kubwa litapata ushindi wa kishindo. Sasa wanachoogopa ni nini kama sio tu kwamba wanataka kuurefusha mjadala ili wakae Dodoma kwa siku nyingi na kuvuna posho zaidi?
 
Tatizo ni kwamba kundi kubwa hawaaminiani--ni kama fisi 100 wanaogombea mzoga wa sungura. Wale wanaobahatika kula nyama hawaaminiwi na wale wanaokosa nyama. Lakini pia wale waliokula nyama wanaweza kugeuzwa kitoweo na wale waliokosa ikiwa watakula na kusahau kujilamba damu yote midomoni mwao. Wale fisi waliokosa nyama wakiona damu midomoni mwa wale waliokula nyama watadhani kwamba ni kipande cha nyama, na hivyo kuanza kuwashambulia kwa lengo la kukikwapua. Zikishatoka damu zaidi, tayari fisi wenzao watageuzwa kitoweo.
 
Hiyo ndiyo tabia ya kifisi inayowakumba wajumbe wa kundi kubwa. Hawaaminiani hata kidogo na wako tayari kugeuzana kitoweo wakati wowote!
 
Ikiwa hali ndiyo hii, itakuwa jambo la busara ipigwe kura ya siri kwani hilo lisipofanyika tutashuhudia 'fisi' hawa wakitupotezea muda sana na kuendelea kutafuna pesa za umma bila huruma. Hivyo basi ipigwe kura ya siri kuamua utata huu uliojitokeza ili zoezi la utungaji wa katiba liishe kwa siku na gharama zilizopangwa badala ya kuendelea kuwatia hasara watanzania kwa mivutano isiyoisha.
 
 

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments